……………….NA TIGANYA VINCENT WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imelipatia ufumbuzi tatizo la kusuasua kwa masoko ya pamba nchini baada ya kufanya mazungumzo na wadau muhimu wa zao hilo na kufikia muafaka.Lengo ni kutaka kuhakikisha pamba yote inanunuliwa ifikapo mwaka mwishoni mwa Mwezi huu na wakulima wanalipwa pesa zao zote.Ameyasema hayo leo (Jumatatu 15, 2019) wakati akizungumza na wakulima wa pamba katika Kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga .Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na Benki Kuu na Benki mbalimbali ili ziweze kuzikopesha Kampuni mbalimbali za ununuzi wa pamba ili zihakikishe zinanunua pamba yote ya wakulima nchini.Alisema wamefanya mazungumzo na wanunuzi wa pamba,Wakuu wa Mikoa inayolima pamba,viongozi wa mabenki na Gavana wa Benki kuu na kufikia makubaliano.Waziri Mkuu alisema wanunuzi walishindwa kununua pamba yote kwa pesa zao kwa vile hawakuweza kukopeshwa na benki ambayo nayo hayakuhakikishiwa dhamana na Benki kuu.Alisema baada ya mazungumzo wamekubaliana Benki kuu ya Tanzania kuanza kutoa dhamana kwa benki ambayo nazo zitatakiwa kutoa mikopo kwa wanunuzi wa pamba.Alibainisha makubaliano hayo sasa yanafungua mlango wa wanunuzi kununua pamba yote ya wakulima tena kwa pesa taslimu na sio mkopo.Aidha Waziri Mkuu,aliwaonya wanunuzi kutotumia pesa wanayopata kufanya mambo tofauti na badala yake waitumie kununulia pamba pekee.Waziri Mkuu aliwapongeza wakulima kwa kuzalisha na kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 135,000 mwaka 2017,mwaka 2018 tani 220,000 na mwaka huu wanatarajia kupatikana tani zaidi ya 300,000.Kwa upande wa Waziri wa Kilimo,Japhet Hasunga alisema uzalishaji wa pamba msimu huu unaweza kuongezeka hadi kufikia tani kati ya 300,000 hadi 350,000.Aidha alisema maghala mengi ya pamba hayana ubora na kwamba wanafanya jitihada kuhakikisha yanakuwa na ubora sio kama ilivyo sasa.Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Aggrey Mwanri,alisema wamefanikiwa kuwafanya wakulima walime kwa tija kwa kuongeza uzalishaji kwa kilo kutoka kilo 300 hadi 800 kwa ekari.Awali Mkuu wa Wilaya ya Igunga,John Mwaipopo,alisema wakulima walikuwa bado hawajapeleka pamba zikiwa bado majumbani huku wale waliopeleka ghalani,kuwa bado hawajalipwa.Mbunge wa jimbo la Manonga,Seif Gulamali alisema kuwa wakulima wana hali mbaya kutokana na kutouza pamba yao na hivyo kushindwa kufanya mambo ya msingi kama kujikimu kwa chakula na gharama zingine za maisha.Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewashauri wakulima wa mazao mbalimbali hapa nchini kujenga utaratibu wa kuweka mipango mizuri ya kujiandaa ya kilimo kijacho kwa kuweka akiba kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo.Alisema Serikali haiwezi kutoa pembejeo kwa kila zao la Mkulima hapa nchini badala yake ni jukumu la wakulima kujenga utaratibu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya uboresahaji wa kilimo kijacho
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mikokoteni iliyosheheni pamba wakati alipotembelea ghala la Chama cha Msingi cha Ushirika cha kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga alikofanya ziara ya siku moja ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, Julai 15, 2019. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).