Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally akizungumza na wanachama wa Tawi la Oloshonyokie Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya kulizindua na kuchangia mabati 100.
Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally akishiriki ujenzi wa ofisi ya CCM Tawi la Songambele Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambapo alichangia mabati 100.
……………………….
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt Bashiru Ally Kakurwa ameyapatia mabati 200 matawi ya CCM ya Oloshonyokie Naisinyai na Songambele Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa ajili kujenga ofisi mpya za matawi hayo.
Dk Bashiru akizungumza na wanachama wa matawi hayo alisema mabati hayo 200 yanatolewa kupitia mfuko wa kuendeleza chama wa Mwenyekiti wao Rais John Magufuli.
Alisema uhai wa chama hicho unategemea wanachama waliopo kwenye matawi na mashina hivyo wanayaunga mkono ili kuendelea kuifanya CCM iwe karibu zaidi na wananchi.
Pia, aliwapongeza baadhi ya wadau wa maendeleo wa mji mdogo wa Mirerani, ambao ni wana CCM, Paul Mollel na Siria Mepukori kwa kila mmoja kuchangia sh500,000 ya ujenzi wa tawi la CCM Songambele na diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardad) alijitolea mifuko 20 ya saruji kwa tawi la Songambele.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alijitolea mifuko 100 ya saruji ya tawi la Songambele, mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya alijitolea mifuko 40 kwenye tawi la Oloshonyokie na mifuko 20 ya saruji katika tawi la Songambele.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Yefred Myenzi alisema yeye binafsi anachangia mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa tawi la CCM Songambele.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Millya alisema amewatafutia wadau na amewachangia kwani matawi yote ni ya kwake, Naisinyai yote ni CCM japo hapo Songambele diwani ni Chadema.
Kada wa chama hicho Siria Mepukori alisema yeye ni mdau wa maendeleo na aliamua kumuunga mkono Dk Bashiru kwa sh500,000 ili kufanikisha ujenzi wa tawi hilo la Songambele.
Kada mwingine Paul Mollel alisema amechangia sh500,000 kwenye ofisi hiyo ya Songambele ili kumuunga mkono Katibu Mkuu wa CCM ambaye ana lengo zuri la kuhakikisha matawi yanajengwa.