Ng’ombe aina ya Sahiwal walioko Transamara nchini Kenya walioboreshwa kupitia Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.
Mratibu wa Mradi wa Sahiwal kutoka Tanzania, Dk. Zebron Nziku akimpongeza mfugaji wa ng’ombe wa Wilaya ya Kiligoris, Transmara nchini Kenya, Oltetia Ole Oltetia kutokana na juhudi kubwa alizofanya kuboresha mifugo yake.
Wafugaji wa Tanzania na Kenya wakijadiliana kwa pamoja namna bora kuboresha ufugaji wao wakiwa kwenye mafunzo katika Chuo cha Uchakataji Maziwa (DTI), Naivasha Kenya
Wafugaji wa Tanzania na Kenya walioko kwenye mafunzo nchini Kenya wakiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa Mradi wa Sahiwal , Dk Zebron Nziku na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kutembelea Chuo cha Uchakati Maziwa(DTI), Naivasha Kenya
Afisa Mtafiti wa Mifugo Mkuu (PLRO), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Hassan Mruttu akisalimiana na mfugaji aliyeko kwenye mradi wa Sahiwal, Kantet Ole Kate wa Transmara Narok nchini Kenya mara baada ya wafugaji wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa ziara ya mafunzo
Mratibu wa Mradi wa Sahiwal Tanzania, Dk. Zebron Nziku wa mwisho kulia akiwa katika picha ya pamoja na wafugaji wakiwa mpaka wa Namanga muda mfupi kabla ya kuingia nchini Kenya kwa ziara ya mafunzo.
Na Mwandishi Wetu, Transmara Kenya
WAFUGAJI wa Tanzania kupitia Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe aina ya Sahiwal wako nchini Kenya kwa ziara ya mafunzo yaliyoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.
Wafugaji hao kutoka Umoja wa Wafugaji wa Sahiwal Longido (UWASALO) wamekutana na wafugaji wa Transmara nchini Kenya wanaonufaika na ufugaji kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji na kuhifadhi na uendeleza nyanda za malisho ya mifugo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea wafugaji wa ng’ombe aina ya Sahiwal katika eneo la Kilgoris -Transmara, nchini Kenya, Mratibu wa Mradi huo wa Sahiwal kutoka Tanzania, Dk. Zebron Nziku amesema ziara hiyo imekuwa na tija kubwa kwa wafugaji wa Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya mageuzi makubwa katika uboreshaji Koosafu za Mifugo.
Dk. Nziku amesema mradi huo tayari umeendesha mafunzo yaliyohusisha wataalam na wafugaji kutoka Halmashauri ya Longido nchini Tanzania kwa ushirikiano na wafugaji wa Transmara nchini Kenya juu ya mbinu bora za uzalishaji na utunzaji wa Sahiwal.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kutoa fursa kwa wafugaji wa Sahiwal kutoka Halmashauri ya Longido nchini Tanzania ambapo mradi huo umetekelezwa kwenda kuona na kujifunza kwa wafugaji wenzao waliofanikiwa kufuga ng’ombe wa aina hiyo kwa muda mrefu nchini Kenya ili kubadilishana uzoefu hasa katika eneo la uzalishaji kwa njia ya uhimilishaji.
Alisema mradi huo umetekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania na Kenya kwa lengo la kuelimisha wafugaji, namna bora na rahisi ya kuzalisha na kutunza wa ng’ombe wa Sahiwal kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji
Dkt. Nziku alisema Sahiwal ni ng’ombe wanaopatikana kwenye nchi zote ndani ya Afrika Mashariki (transboundary breed) na wana uwezo wa kutoa nyama nyingi na maziwa kati ya lita 14-16 kwa siku, hivyo mradi umelenga kuboresha, kuendeleza na kutunza Mbari (breed) za ng’ombe wa Sahiwal ili kuboresha maisha ya wafugaji kupitia mifugo hiyo.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Tanzania mradi huu umefanikiwa kununua Madume bora Matatu ya Mbegu za Sahiwal ambayo kwa sasa yamehifadhiwa kwenye Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji NAIC -Arusha kwa ajili ya kutoa mbegu zitakazo wanufaisha wafugaji wengi zaidi nchini.