Mmoja wa walimu waliohudhulia wakisisitiza suala la ukosefu wa makazi kuwa kikwazo kwa walimu hasa maeneo ya vijijini.
Mdau wa Elimu mmiliki wa Cannan School Bw. Asanga Ndile akiwasilisha hoja ya kukosekana kwa vitabu vya kiada kwa shule za mchepuo wa kingereza
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa Elimu wakifuatilia mada zilizowasilishwa, pichani wanafunzi wa shule mbalimbali za wilaya ya mbozi waliofanya vizuri wakisubiri kuzawadiwa kwenye mkutano huo.
******************
Na Danny Tweve -Songwe
Wadau wa Elimu Wilayani Mbozi katika Mkoa wa Songwe wametahadharisha kuwa, jitihada za kuinua ufaulu wilayani Mbozi zinaweza kukwama ikiwa pengo la walimu wa madarasa ya awali lililopo sasa halitashughulikiwa.
Takwimu zilizowasilishwa jana na afisa elimu wa wilaya hiyo Bi Hosana Nshullo zinaonyesha kuwa wilaya ya mbozi hakuna mwalimu hata mmoja kwa ngazi ya elimu ya awali na kuwepo upungufu wa walimu 563 kwa wilaya nzima.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya elimu wilayani humo afisa elimu Bi Nshullo amesema mahitaji hayo yanapaswa kushughulikiwa kwakuzingatia kuwa madarasa ya awali ni sehemu muhimu ya makuzi ya watoto kwaajili ya kuwaandaa kuelekea ngazi za juu.
Wakichangia kwenye mkutano huo, baadhi ya washiriki wameonyesha pia hofu yao juu ya hali ya upungufu wa nyumba za walimu hasa maeneo ya vijijini na kuomba jitihada zinazofanyika sasa za usimamizi wa ujenzi wa vyoo na madarasa zielekezwe pia kwenye nyumba za walimu
Mwalimu Modestus Kalinga kutoka shule ya msingi Ihanda ameelezea kuwa uhaba wa nyumba za walimu unahitaji kutazamwa kwa upana kwani, miundombinu ya shule ni pamoja na nyumba za walimu na kwamba miongoni mwao wanaishi kwenye makazi duni.
Katika kujibu hilo Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi bi Isabela Mbaya alidokeza kuwa halmashauri yake itaingiza mpango wa makazi ya walimu kwenye awamu inayofuata baada ya kukamilisha kwa kampeni ya vyoo mashuleni ambayo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake mdau mwingine wa elimu bwana Asanga Ndile amesema pamoja na kuangalia changamoto za miundombinu ni vyema pia matatizo ya kukosekana kwa vitabu kwa shule za English medium ni eneo muhimu linalotakiwa kuangaliwa.
Alisema kwa muda mrefu vitabu vya kiada kwa shule za mfumo wa Kingereza limwakuwa likiathiri utendaji wa shule hizo hivyo wakati Fulani kusababisha watoto kukosa mwelekeo wa nini wanachopaswa kujifunza kutokana na kufanywa eneo la kujaribishia vitabu.
Mkutano huo hufanywa kila mwaka kwaajili ya kujadili mafanikio na changamoto za sekta ya elimu na kuchukua hatua, huku pia ukitumika kuwazawaidia watoto, walimu na shule zilizofanya vizuri kwenye mitihani ya kuanzia darasa la nne, la saba, kidato cha nne na cha sita. Mwisho