Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Utambalila wilayani Mbozi waliohudhulia mkutano wa kumsimamisha mwenyekiti wao wa Kijiji bwana Dotto Kessy Mgalla
Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo akizungumza kwenye mkutano huo, kulia kwake ni bwana Dotto Kessy Mgalla, aliyekuwa mwenyekiti wa Kijiji kabla ya kusimamishwa uongozi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji akiwa amekaa mwishoni mwa benchi la wananchi baada ya kusimamishwa uongozi.
……………………..
Na Danny Tweve -Mbozi
Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo amemsimamisha majukumu yake aliyekuwa mwenyekiti wa Kijiji cha Utambalila Bw Dotto Kessy Mgalla , kata ya Nambinzo wilayani humo baada ya kutuhumiwa na wananchi pamoja na chama chake kilichompa dhamana ya uongozi, kujihusisha na vitendo viovu.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya chama cha Mapinduzi kumwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Mbozi kikielezea hatua za ndani ya chama zilizochukuliwa baada ya bwana Dotto Kessy Mgalla kukaidi kikao kilichohudhuliwa na mwenyekiti wa CCM wilaya kwa lengo la kusikiliza tuhuma zilizowasilishwa kwenye ngazi ya wilaya dhidi yake.
katika hali ya kushangaza wananchi wakitegemea angeomba msamaha, alipopewa nafasi ya kujitetea mbele ya wananchi wake, Bw. Dotto alimweleza wazi wazi Mkuu wa wilaya kuwa hataki tena uongozi amechoka!
Bwana Dotto Kessy mbele ya Mkuu wa wilaya ya Mbozi alieleza wazi kuchoshwa na madaraka ya uenyekiti kutokana na wananchi kumfanya adharaulike kwenye jamii kutokana na tuhuma wanazomshushia mara kwa mara, na akaomba kama kuna maamuzi ya kumwondoa basi ifanyike haraka.
Kutokana na hatua hiyo, mkuu wa wilaya alitangaza mbele ya wananchi kumsimamisha uongozi kwenye ngazi ya kijiji hatua ambayo ambayo bwana Kessy aliridhia na kisha kuondoka zake kwenye kiti.
Miongoni mwa malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi kwenye mkutano huo ni pamoja na kuwepo matukio mengi ya wizi wa ng’ombe ambapo yeye kama kiongozi hakuonekana akichukua hatua zozote ikiwa ni pamoja na kushindwa kuhamasisha vijana kufuatilia ng’ombe zilikoelekea.