Moja ya gari ambalo limefungwa mfumo wa gesi asilia na kuanza kutumika
**************
NA EMMANUEL MBATILO
Imeelezwa kuwa Ufungaji wa mfumo wa gesi asilia kwenye magari yanayotumia petrol inaweza kumsaidia mmilikia au mtumiaji wa gari hilo kuondokana na gharama za mafuta kwa kiasi kikubwa.
Amesema hayo leo Afisa Mtafiti wa TPDC, Bw.Sylvanus Malimi katika maonesho ya biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kiwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Fullshangwe blog, amesema kuwa kuna urahisi kutumia gari ambalo linatumia mfumo wa gesi asilia kwani kuna uwezo wa kupunguza gharama za mafuta pamoja na uharibifu wa mazingira na mfumo huo unalifanya gari kubaki na ubora wake ili hali likiongezeka ufanisi.
“Kwasasa gari zote zinazotumia petrol zinaweza kufungwa mfumo wa gesi asilia ili mradi ziwe katika hali nzuri”. Amesema Bw.Malimi.
Ameongeza kuwa watumiaji wa magari wanatakiwa wapate elimu ya kutosha katika matumizi ya magari yatumiayo mfumo wa gesi asilia kwani yamekuwa hayana gharama baada ya ufungaji wa mfumo wa gesi asilia.
Aidha amesema kuwa TPDC wanampango wa kuongeza vituo vya kujaza gesi asilia katika magari yaliyofungwa mfumo wa gesi asilia baada ya kuwa na kituo kimoja ambacho kipo Ubungo Maziwa barabara inayopitia kati ya kiwanda cha Chibuku na Twiga Cement depot.