Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Dkt. Upendo Mwingira akifungua mafunzo ya Kimataifa ya uchukuaji wa Takwimu za ugonjwa wa Vikope(Trakoma) yanayofanyika jijini Arusha
Wataalam wa Macho kutoka mataifa mbalimbali wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya afya,wadau mbalimbali wa macho nchini pamoja na nchi mbalimbali Duniani zikiwemo Afrika Mashariki,Magharibi na Kati
Afisa Mpango kutoka NTD anayeshughulika na Trakoma Bi.Alistidia Simon akiwakaribisha wataalam wa macho kwenye mafunzo hayo
Mratibu wa NTD Mkoa wa Arusha Mwanahawa Kombo akitoa salamu za mkoa kwa niaba Mganga Mkuu wa Arusha.Mafunzo haya hapa nchini yanafanyika kwa miaka mitatu mfululizo
………………………………………
Na.WAMJW,Arusha
Tanzania imeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Trakoma kutoka wilaya 71 hadi
sita ambazo zitaendelea na umezaji kingatiba
Hayo yamesemwa leo na Mratibu wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya Dkt.Upendo Mwingira wakati wa mafunzo ya Kimataifa ya uchukuaji wa takwimu za ugonjwa wa vikope(Trakoma) yanayofanyika jijini hapa.
Dkt.Mwingira amesema kuwa kama nchi inajivunia kwa mafanikio makubwa kwani hivi sasa wilaya 65 hazihitaji tena kingatiba kulingana na vigezo vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Lengo la WHO hadi ifikapo mwaka 2020 tuwe tumeweza kutokomeza ugonjwa wa Trakoma kama tatizo la kijamii,kwamba hatutaki maambukizi mapya”Alisisitiza Dkt.Mwingira.
Aidha,alisema mwaka 2010 katika tathimini Tanzania kulikua na makadirio ya wagonjwa wa vikope takribani 160,000,lakini kutokana na jitihada za Wizara ya Afya hadi Julai 2018 inakadiriwa wagonjwa hao wamepungua mpaka kufikia 17,000.
Hata hivyo Dkt.Mwingira alisema zoezi la kusawazisha vikope hapa nchini linaendelea zaidi ya mikoa kumi sasa hivi katika halmashauri zenye maambukizi.
Mafunzo haya yanahusisha wataalam wa macho kutoka mataifa mbalimbali Duniani na kwa nchi za Afrika yanahudhuriwa na nchi za afrika Mashariki,Magharibi na Kati.