TIMU za Algeria na Madagascar zimefanikiwa kuingia Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 baada ya kuwatoa Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumapili.
Uwanja wa Juni 30 mabao ya Algeria yalifungwa na mshambuliaji wa Esperance ya Tunisia, Mohamed Youcef Belaili dakika ya 24, nyota wa Manchester City ya England, Riyad Mahrez dakika ya 57 na kiungo wa Napoli ya Italia, Adam Ounas dakika ya 82.
Katika mchezo wa kwanza, Madagascar iliitupa nje Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 2-2 Uwanja wa Alexandria nchini Misri.
Dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana 2-2, mabao ya Madagascar nchi anayotoka Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad yakifungwa na kiungo wa MC Alger ya Algeria, Ibrahim Amada dakika ya tisa na mshambuliaji wa Clermont ya Daraja la Pili Ufaransa, Faneva Ima Andriatsima dakika ya 77.
Mabao ya DRC yalifungwa na mshambuliaji wa Beijing Guoan ya China, Cedric Bakambu dakika ya 21 na mlinzi wa Porto ya Urenoi, Chancel Mbemba dakika ya 90 kwa kichwa kufuatia kona ya mshambuliaji wa TP Mazembe, Meschak Elia dakika ya 90.
Katika mikwaju ya penalti, Ibrahim Amada, Romain Metanire wa Minnesota United ya Marekani, Thomas Fontaine wa Reims ya Daraja la Pili Ufaransa na Jerome Mombris wa Grenoble Foot 38 ya Ufaransa wote walifunga.
Upande wa DRC waliofunga ni Bakambu wa Beijing Guoan ya China na Paul-Jose M’Poku Ebunge wa Standard Liège ya Ubelgiji, wakati Marcel Tisserand wa Wolfsburg na Yannick Bolasie wa Everton walikosa.
Algeria na Madagascar zinaungana na Senegal, Benin, Nigeria na Afrika Kusini zilizotangulia katika hatua hiyo.
Hatua ya 16 Bora inakamilishwa Leo kwa mechi mbili; Mali na Ivory Coast na Ghana dhidi ya Tunisia Uwanja wa Ismailia.