************
Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mh Rais Dr John Pombe Magufuli imejizatiti katika kutekeleza mpango kabambe wa kuwajengea Ujuzi Vijana kwa lengo la kutatua changamoto ya Ajira ili kupitia ujuzi watakaoupata katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa chini ya Programu ya kukuza ujuzi inayosimaniwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hayo yamesemwa leo Mirerani,Wilaya ya Simanjiro-Manyara na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde wakati wa Kongamano la Wajasiriamali na shindano la kusaka vipaji linaloratibiwa na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Manyara Mh Esther Mahawe ambapo Naibu Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo kuelezea mipango mbalimbali ya Serikali katika kuwajengea ujuzi Vijana wa Kitanzania kupitia program ya kurasimisha ujuzi,mafunzo ya kilimo cha kitalu nyumba na mafunzo kupitia vyuo vya Ufundi yote yenye lengo la kumjengea uwezo wa ujuzi kijana wa kitanzania ili aweze kujiajiri mwenyewe na kuajiri Vijana wengine.
“Ni mpango mkakati wa serikali pia kuwajengea uwezo Vijana wa Mirerani kupata ujuzi wa kuongeza thamani katika madini ya Tanzanite ili kuongeza fursa zaidi za Ajira zitokanazo na sekta hii ya madini”Alisema Mavunde
Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Mbunge Wa Viti Maalum Mh Esther Mahawe ameeleza mikakati yake katika kuwakomboa wakina Mama na Vijana wa Mkoa wa Manyara kwa kuendelea kutoa elimu ya kujitambua na Ujasiriamali sambamba na kuchangamkia fursa zilizopo mkoani hapo.
Kongamano hilo lilikwenda sambamba na shindano fupi la kutafuta vipaji vya wasanii ambao watalelewa na kufadhiliwa na Ofisi ya Mbunge Esther Mahawe.