Katibu wa UWT, Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa,akizungumza na washiriki wa mafaunzo ya ujasirimali kwa wanawake ambayo yaliwashirikisha wataalamu kutoka SIDO na Ofisi ya maendeleo ya jamii.
Afisa Uendelezaji Biashara kutoka SIDO,akitoa elimu kwa washiriki wa mafaunzo ya ujasirimali kwa wanawake ambayo yaliwashirikisha wataalamu kutoka SIDO na Ofisi ya maendeleo ya jamii.
Mratibu Dawati la Uwezeshaji wananchi kutoka jiji la Dodoma Bi.Hidaya Mizega akitoa elimu na mbinu kwa washiriki wa mafaunzo ya ujasirimali kwa wanawake ambayo yaliwashirikisha wataalamu kutoka SIDO na Ofisi ya maendeleo ya jamii.
Mjumbe Kamati ya Utekelezaji UWT Dodoma Mjini Mwl.Saphia Mfaki,akizungumza na washiriki wa mafaunzo ya ujasirimali kwa wanawake ambayo yaliwashirikisha wataalamu kutoka SIDO na Ofisi ya maendeleo ya jamii.
………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
ZIARA ya Umoja wa Wanawake Wilaya ya Dodoma Mjini ya kutoa elimu kuhusu ujasiriamali kwa Wanawake imehitimishwa leo katika Kata za Mihuji, Makole na Uhuru.
Akizungumza katika mafunzo hayo ya ujasiriamali Katibu wa UWT, Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa amesema kupitia ziara hiyo ambayo iliwahusisha wataalamu kutoka SIDO na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake wameweza kunufaika na Elimu hiyo ya ujasiriamali.
” Tumekua na ziara kwa kata 41 za Jiji la Dodoma, kote huko tulizunguka na kuzungumzia na akina Mama kuhusu elimu ya kujitegemea na kujikwamua na umaskini.
” Tunampongeza na Kumshukuru Rais wetu Dk Magufuli, kwa kuondoa riba katika mikopo inayotolewa na Halmshauri za Wilaya Nchini kwa wanawake, vijana na walemavu lakini haswa tunamshukuru kwa kuwakumbuka walemavu ambao ni kundi lililokua limesahaulika katika suala zima la mikopo.
” Kuna fursa nyingi sana hivi sasa jijini Dodoma hasa baada ya Rais kuturasimisha kuwa Makao Makuu ya Nchi na Jiji, ni jukumu letu kama UWT kuandaa mafunzo na warsha mbalimbali za kuwakomboa Wanawake kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi,” amesema Diana.
Amesema ziara hiyo imekua na mafanikio makubwa kwani imechangia idadi kubwa ya wanawake kujiunga katika vikundi vidogo vidogo ambavyo vitawasaidia kupata mikopo Jiji huku wengine wakienda SIDO kupata mafunzo kamili ya fani mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Uendelezaji Biashara SIDO, Crispin Kapinga amesema muamko wa Wanawake katika kujiunga na SIDO ili kupatiwa mafunzo mbalimbali umekuwa ni mkubwa baada ya ziara hiyo ya UWT.
” Hakika UWT Wilaya ya Dodoma Mjini, wanastahili pongezi. Wamezunguka Kata zote kutoa elimu kwa akina Mama Na Vijana ili waweze kujiajiri fursa ni nyingi sana kwenye Jiji letu hivi sasa.
” Mfano kuna akina Mama ambao baada ya kupata mafunzo haya wamekuja pale SIDO kwenye ofisi zetu kufundishwa jinsi ya kutengeneza mifuko mbadala na sasa uchumi wao umekua mkubwa kutokana na uhitaji wa mifuko hiyo kwa saa, nitoe rai kwa Taasisi nyingine kuiga mfano huu wa UWT katika kutoa elimu kwa vijana na akina mama,” amesema Kapinga.
Nae Hidaya Mizega ambaye ni Mratibu dawati la uwezeshaji Jiji la Dodoma, amewataka wanawake Wilayani humo kujitokeza kwa wingi katika kuchukua mikopo inayotolewa na Manispaa ya Jiji la Dodoma kwa Wanawake, Vijana na Walemavu.
“Tunapaswa kuwashukuru UWT Wilaya ya Dodoma kwa kuandaa mafunzo haya, ni ombi langu kwenu akina Mama kujihamasisha nyie wenyewe pamoja na watoto wenu kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili kuweza kupatiwa mikopo.
” Wanawake ndio uti wa mgongo wa Familia, hampaswi kuwa tegemezi, tuamke tuzikimbilie fursa lakini tusiamke peke yetu, tuwashike mikono na Vijana wetu waache kukaa vijiweni,” amesema Hidaya.
Mmoja wa akina Mama waliohudhuria Mafunzo hayo, Amina Abdallah ameushukuru Uongozi wa UWT Wilaya ya Dodoma kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewafungulia njia katika kujikwamua kiuchumi.