WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo ameonyesha kukerwa na kasi ndogo iliyoonyeshwa na watendaji katika kukamilisha miradi ya afya na elimu iliyopata fedha wilayani Kisarawe.
Waziri Jafo ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea katika Shule za sekondari zikiwemo Sekondari za Kibuta, Kurui, Mzenga, na Kimani, pamoja na ukarabati wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe alipofanya ziara ya kikazi Jimboni kwake kukagua miradi ya maendeleo.
Amewataka watendaji wote hususani Mkurugenzi na wakuu wake wa Idara kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa wananchi wanataka huduma kutoka kwenye serikali yao ambayo inajitahidi kuleta fedha ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Awali, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe, Mussa Gama amekiri kuchelewa kwa miradi hiyo kutokana na upatikanaji wa vifaa hususani saruji.
Hata hivyo amemhakikishia Waziri Jafo kwamba watafanya kila liwezekano ili miradi yote iwe imekamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.