Mtoa huduma kwa wateja wa Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) akiwahudumia
wateja mbalimbali waliofika katika Banda la Shirika hilo kwa ajili ya kupata taarifa
kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa wakati wa Maonesho ya Biashara ya
Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam.
Mtoa huduma kwa Wateja katika Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) Halima Mtui
akimhudumia mmoja wa wateja waliofika katika Shirika hilo kwa ajili ya kupata
taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
***************
SHIRIKA la Mawasiliano Nchini (TTCL) katika kipindi cha siku 30 limeweza kusajili wateja wapya 215,000, ikiwa ni Mpango Mkakati wa Shirika hilo katika kujiinua kibiashara na kuongeza wigo huduma ya Mawasiliano kwa Watanzania ikiwa ni utekezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli.
Akizungumza leo Alhamisi (Julai 4, 2019) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Meneja Mawasiliano wa TTCL Nicodemus Mushi alisema Shirika hilo limetekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilolitoa kwa Shirika hilo tarehe 21 Mei, mwaka huu.
Mushi alisema hadi sasa huduma za Mawasiliano za Kampuni hiyo katika Mfumo wa 4G zinapatikana katika Mikoa 16 nchini na mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa maeneo yaliyobaki yanapata huduma za Shirika kupitia Mpango Mkakati wa Shirika hilo uliojiwekea na hivyo kuweza kuleta ushindani wa huduma ya mawasiliano na makampuni mengine nchini.
“Mwaka uliopita tulijiwekea Mpango Mkakati wetu ambao utahakikisha kuwa tunaweza kuleta ushindani na makampuni mengine na hivi sasa kama unavyoona tumeweza kupata wateja wapya 215,000 na kupitia maonesho hayo tutaweza kuongeza wateja wengi zaidi ” alisema Mushi.
Aliongeza kuwa kwa sasa Shirika hilo limeweza kupata wateja wengi zaidi wakiwemo watumishi wa serikali, ambapo kwa kutambua umuhimu huo, TTCL imeanzisha kifurushi maalum cha ‘watumishi pack’ ambacho kinaweza kutumiwa na wafanyakazi wote wa serikali kwa kuweza kukamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo vitambulisho vya kazi.
Akifafanua zaidi Mushi, alisema kauli zinatolewa na watu mbalimbali kuhusu kauli ya Rais Dkt. John Magufuli kuwataka wafanyakazi wa serikali kutumia huduma za mawasiliano za shirika hilo, ni kuwa zitawahusu watumishi wa umma ambao wanalipiwa huduma za mawasiliano ya simu na serikali na si kinyume na maelekezo hayo.
Aliongeza kuwa malengo ya Taasisi hiyo ni kuweza kujipanga ili kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango ili kuweza kuongoza na kuwa kampuni bora ya mawasiliano inayotoa huduma bora kwa wateja wake nchini.
“Sisi kwa upande wetu tumeendelea kuwalipa vizuri mawakala wetu ikiwemo kutoa kamisheni nzuri kwao ili kuhakikisha kuwa huduma zetu zinazotolewa zinakuwa zinakidhi matakwa ya wateja na soko la mawasiliano kwa ujumla” alisema Mushi.