Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa MDA wakifuatilia mada mbalimbali juu ya uwekezaji wilayani Makete
Festo Sanga kushoto akiwa na washiriki wengine kwenye mkutano huo wakimsikiliza mkurugenzi wa kituo cha Uwekezaji Bw. Geofrey Mwambe juu ya fursa zilizopo wilayani Makete
***********
Na Danny Tweve-
Mianzi
Wilaya ya Makete inajipanga kutumia raslimali zilizomo ikiwemo mianzi kuanzisha viwanda vya usindikaji wa vijiti vya Meno (toothpeak) ambavyo licha ya wingi wa mmea huo katika mikoa ya Iringa na Njombe bado Tanzania imeshindwa kuwa na kiwanda cha aina hiyo.
Mikoa hiyo miwili imekuwa maarufu kwa uzalishaji wa pombe ya Ulanzi ambayo kwa karne sasa licha ya matumizi ya wakazi wake kwaajili ya burudani ya kilevi,bado tafiti za namna ya kusindika hazijaweza kufanikishwa licha ya njia za asili za uhifadhi ambazo hata hivyo hazijaweza kuthibitisha ubora wake.
Akizungumza kwenye mkutano wa Chama cha Maendeleo Makete (MDA) uliomalizika juzi katika Hotel ya Nefaland jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wake Bw. Clement Sanga, alisema tayari wilaya imeainisha maeneo kadhaa ya uwekezaji ambayo sasa inayawataka wafanyabiashara walio nje ya wilaya hiyo kwenda kufungua viwanda.
Kulingana na takwimu kutoka ndaki ya misitu ya Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, Tanzania ina hekta za mianzi 127,824 ambapo kwa nchini kuna jamii nne ambazo kwa pamoja zina uwezo wa kudumu kwa miaka 50 zikitoa faida kwa wazalishaji kwa kipindi chote, hata hivyo bado matumizi yam mea huo bado yamekuwa hayana tija kiuchumi ukiachilia kijamii kwenye burudani yta pombe ya ulanzi.
Miongoni mwa bidhaa za mianzi kulingana na utafiti uliofanywa na ndaki hiyo ni pamoja na samani za ndani kama Makabati, meza, vitanda,vikapu na kwamba zaidi ya bidhaa 1500 zinaweza kutengenezwa na Mianzi. Rwanda katika Afrika ndiyo nchi pekee iliyotengeneza sera ya Muanzi ya 2011 baada ya kutambua faida za mmea huo kibiashara.
Kulingana na Mwenyekiti huyo , baadhi ya viwanda vinavyotajwa wilayani Makete ni pamoja na mahitaji ya kiwanda cha usindikaji wa juisi za matufaa (apple) ambapo wilaya ya Makete ni moja ya maeneo ambayo wafanyabiashara wa matunda wamekuwa wakitangaza kuwa yanatoka nchini Afrika Kusini wakati ukweli yanazalishwa hapa hapa nchini hasa wilaya ya Makete na Njombe.
Katika kutekeleza mkakati huo, Umoja huo umeitisha mkutano huo ukihusisha wafanyabiashara wa jamii ya WanaMakete kutoka maeneo mbalimbali duniani ambako wawakilishi kutoka wafanyabiashara maarufu kama wakinga wanaoishi China walionyesha nia ya kujenga viwanda kwa kutumia teknolojia ndogo ndogo zinazopatikana nchini humo.
Vipaumbele katika hamasa hiyo ni kutumia fursa ya rasrimali zilizopo wilayani humo zikiwemo vyanzo vya maji safi na salama vya asili ambavyo vinaweza pia kutumika kuanzisha viwanda vya maji ya kunywa nay a dawa(drips), umeme wa maji na bidhaa nyingine za mianzi zikiwemo samani za ndani.
Katika ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji TIC Godfrey Mwambe amesema, jukumu la taasisi yake ni kuhakikisha inatafsiri maono ya serikali ya awamu hii ikiwa ni pamoja na kushauri uanzishwaji wa mifumo itakayosaidia ukuaji wa sketa binafsi na kupitia Ubia.
Alisema mtazamo wa Chama cha MDA, kwa sasa wanapaswa kuangalia pia uwekezano wa kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji Makete sambamba na Mfuko wa Maendeleo wa Makete ambapo kupitia vyombo hivyo vitasaidia kukuza shughuli za uwekezaji wilayani wilayani humo.
Ametolea mfano fursa zilizopo kwenye Hifadhi ya Kitulo, kuwa bado hazijatumika vyema kutokana na namna hifadhi hiyo ilivyoanza kupata umaarufu kutokana na upatikanaji wa maua na mimea ambayo watu kutoka nje wanatamani kufika na kutumia bustani hiyo kwa mapumziko ingawa bado hakuna hoteli zenye mvuto kwenye ukanda huo.
Mkutano huo wa Mwaka wa Chama cha Maendeleo Makete kwa mwaka 2019 umedhaminiwa na Benki ya NMB na umeshirikisha wanachama kutoka mikoa yote ya Tanzania na wawakilishi wa wafanyabiashara wana-Makete kutoka nchi za China na Hong Kong ambako wamejiimarisha zaidi kibiashara.