***********
Na Danny Tweve Songwe
Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali CAG itaanza kutoa hati mbili za ukaguzi badala ya moja ya awali kuanzia ukaguzi wa mwaka wa fedha 2019/2020 kwa mamlaka za serikali za mitaa, serikali kuu, wakala na mashirika na taasisi za umma.
Akiwasilisha maoni ya jumla kwenye baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali –CAG, Mkaguzi Mkazi wa Mkoa wa Songwe Bwana Abiud Sanga amesema, hati hizo zitahusu Uzingatiaji wa Kanuni, Miongozo, Sheria na taratibu za fedha.
Alifafanua kuwa hati nyingine itahusiana na Mpangilio wa vitabu vya mahesabu kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa.
Halmashauri ya wilaya ya Mbozi ni miongoni mwa halmashauri zilizopata hati safi mfululizo katika kipindi cha miaka mitatu ukiwemo mwaka uliofanyiwa ukaguzi wa 2017/2018.
Katika kaguzi zilizopita, ofisi ya CAG ilitoa hati moja kwa kila mamlaka katika madaraja ya hati inayorishisha(unqualified opinion), hati ya mashaka(qualified), hati isiyoridhisha(adverse) na Hati Mbaya(Disclaimer).
Katika kikao hicho, Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwangela, amezitaka halmashauri kuachana na dhana ya kuwa mabingwa wa kujibu hoja na badala yake wanatakiwa kuepuka kusababisha hoja ikiwa ni pamoja na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
Alisema hatua zilizoanza kuchukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji kwa kushirikisha madiwani na Mkuu wa wilaya katika kusimamia miradi, itasaidia kuzuia athari za matumizi mabaya ya fedha zinazoelekezwa vijijini hatua ambayo ni mwanzo mzuri kuelekea kuepuka hati mbaya.
Katika hatua nyingine Baraza hilo limeiomba ofisi ya Mkuu wa mkoa kutoa mrejesho wa matokeo ya ukaguzi maalumu uliofanywa kwenye bodi ya Kahawa ambapo kwa muda mrefu kumekuwepo malumbano kwenye halmashauri hiyo kuhusiana na deni la ushuru wa Kahawa iliyouzwa kutoka Mbozi ambalo limekuwa likitumika kushambuliana kisiasa.
Mwenyekiti wa Halmashauri Elick Ambakisye alisema, ikiwa ofisi ya Mkuu wa mkoa itasaidia kupatikana taarifa hiyo kwenye kikao kijacho cha baraza itasaidia kujenga ushirikiano wa pamoja miongoni mwa madiwani wenyewe na wananchi kutokana malumbano ya muda mrefu yakiwatuhumu miongoni mwao kushirikiana na bodi ya Kahawa.
Akifafanua uwasilishaji wa taarifa hiyo, Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia jenerali Mwangela ameahidi kuileta taarifa hiyo kwenye kikao kijacho, hata hivyo akaagiza Halmashauri kusainiana na Bodi ya Kahawa juu ya ukomo wa muda wa deni kwa fedha zisizokuwa na utata wakati maeneo yenye utata yakiendelea kufanyiwa kazi na vyombo vingine ikiwemo TAKUKURU.
Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya wilaya ya Mbozi ilikuwa na hoja za ukaguzi 41 ambapo hadi sasa jumla hoja 18 zimefungwa huku zingine 23 zikiwa kwenye hatua za uhakiki na utekelezaji, huku maagizo 03 kati ya 07 yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya hesabu za serikali za mitaa LAAC yakiwa yametekelezwa.