Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) wakielekea katika eneo lenye mazalia ya mbu wanaosababisha homa ya Dengue, zoezi limefanyika katika eneo la Msisili Manispaa ya Kinondoni.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiongoza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika Manispaa ya Kinondoni
***************
Na WAMJW-DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. @ummymwalimu leo ametembelea katika Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa Mikoa/Halmashauri ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Dengue.
Katika ziara hiyo Waziri @ummymwalimu ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zinazochukuliwa na Manispaa ya Kinondoni za kupambana na Ugonjwa wa Homa ya Dengue hali iliyochangia kupungua kwa Idadi ya Wagonjwa kutoka Wagonjwa 604 Mwezi Mei hadi kufikia Wagonjwa 450 Mwezi Juni.
“ Nafurahi kuona kwamba idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue katika Wilaya ya Kinondoni, Mwezi Mei kulikuwa na Wagonjwa ambao wamepima na kuthibitishwa 604, lakini mwezi wa tano Wagonjwa wamepungua hadi 450” Alisema Waziri Ummy
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, takwimu za Kitaifa za Wizara ya Afya, mwezi Mei tulikuwa na idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue 3170, na wamepungua Mwezi wa Sita hadi kufikia Wagonjwa 1446, hali inayotoa matumaini katika kuimaliza vita hii ya homa ya Dengue.
Aidha, Waziri Ummy amewapongeza Watendaji wa Sekta ya Afya katika Manispaa ya Kinondoni kwa hatua wanazoendelea kuchukua, ikiwemo kununua Viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu na kununua mashine mpya za kupuliza dawa (motorised sprayers), katika maeneo yenye mazalia ya mbu.
Mbali na hayo, Waziri Ummy amesisitiza juu ya ushiriki wa Wananchi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa homa ya Dengue, huku akieleza kuwa mapambano dhidi ya mbu wa Dengue yatasaidia kupunguza magonjwa mengine kama Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano.
“Ushiriki wa Wananchi ni muhimu sana katika kupambana na ugonjwa wa Dengue, tukipambana na Dengue, kwa upande mwingine tunakuwa tunapambana na ugonjwa wa Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano, kwhiyo ni lazima tuhakikishe kila mtu anashiriki katika kupambana dhidi ya mbu.” Alisema Waziri Ummy.
Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Maulid Mtulia amekazia kwa kuwahasa Wananchi juu ya ushiriki katika vita hii dhidi ya ugonjwa wa Dengue na kusisitiza kuwa Serikali haiwezi kushinda vita hii bila ushirikiano wa Wananchi.
Nae, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamin Sitta amesema kuwa Jumla ya shilingi Milion 132 kwaajili ya zoezi lakutokomeza homa ya Dengue, 90 zimetumika kwaajili ya zoezi zima la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, huku 42 kwaajili ya kununua Mashine za kubwa ya upuliziaji wa dawa hizo.
“Tumetumia gharama ya takribani Milion 90 kwaajili ya upuliziaji katika kila kata na tupo mbioni kuongeza Milioni 42 kwajili ya mashine kubwa yenye uwezo wa kusambaza mara moja kwa kata 10, kwahiyo kwa ujumla tutakuwa tumetumia takribani Milion 132 kwaajili ya zoezi la kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa wa Dengue.” Alisema Mhe. Benjami Sitta.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Festo amesisitiza kuwa Huduma za vipimo vya homa ya Dengu zinapatikana katika vituo vya Serikali vya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo na vituo binafsi bei elekezi isizidi shilingi 50,000/
“Huduma hizi za vipimo zinapatikana kwenye vituo vyetu, na katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo, lakini katika vituo binafsi, bei elekezi isizidi 50,000/ kwa kipimo cha Dengue” alisema Dkt. Festo
Pia, amewaasa Wananchi kuwahi katika vituo vya Afya, pindi waonapo dalili za ugonjwa wa homa ya Dengue na kuachana na mawazo potofu ya matibabu ya Dengue kama majani ya mpapai kwani yanawezapelekea kupata matatizo mengine yakiafya.