***********
Katika kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali
inaendelea, pamoja na mambo mengine, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na
ufanyaji biashara katika sekta mbali mbali hapa nchini, ikiwemo sekta ya
usafirishaji. Sekta hii ni miongoni mwa Sekta zenye mchango mkubwa katika
kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, sekta hii imekuwa ikichangia pia kuzalisha ajira kwa vijana wetu katika nafasi mbali mbali kama vile Madereva, Mafundi na kada nyingine nyingi.
Pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na sekta hii, zipo changamoto kadhaa
ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na Serikali kwa kushirikiana na wadau.
Kwa upande wa utekelezaji wa Sheria za Kazi, changamoto zimeendelea kujitokeza katika masuala ya Mikataba ya Ajira, Malipo ya Mishahara na Posho mbali mbali, ambapo imebainika yapo Makampuni machache yanayolenga kuchafua kazi nzuri inayofanywa na sekta hii, ambapo makampuni hayo machache yamekuwa yakifanya udanganyifu kwenye Mikataba ya Ajira za Madereva wao pindi yanapofanya maombi ya Leseni za Usafirishaji.
Aidha, katika jitihada za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi;
Kitengo cha Usalama Barabarani na LATRA inatarajia kufanya Zoezi Maalum la
Ukaguzi kwa lengo la kukagua Mikataba hiyo na kuangalia utekelezaji wa Sheria
kwa ujumla.
Zoezi hili linatarajiwa kufanyika kwa namna mbili tofauti ambapo; (i) Maafisa Kazi
waliopo katika Ofisi za Kazi watapita katika Kampuni zote za Usafirishaji na (ii)
Timu maalum ya Maafisa Kazi wa kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya
Wafanyakazi Madereva, LATRA na Jeshi la Polisi; Kitengo cha Usalama
Barabarani watafanya Ukaguzi wa Mikataba kwenye Vituo Vikuu vya Ukaguzi
kama vile Kituo cha Mabasi Ubungo, Kituo cha Kuegesha Malori cha
Misugusugu na vituo vingine vinavyofanana na hivyo hapa nchini.
Aidha, sambamba na ukaguzi huo, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi
Madereva na Vyama vya Waajiri watapatiwa elimu kuhusu haki na wajibu wao
katika kutekeleza Sheria za Kazi.
Hivyo, ninapenda kuwaarifu Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji, Wafanyakazi
Madereva na Umma kwa ujumla kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu inatarajia kuanza rasmi Zoezi la Ukaguzi wa Mikataba ya
Ajira ya Madereva na Utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa ujumla ifikapo tarehe 15
Julai, 2019.
Ili kulifanya zoezi hili kuwa lenye ufanisi, ni vema Wamiliki wa Vyombo vya
Usafirishaji kuhakikisha kuwa Mikataba ya Madereva wenu inakuwepo katika
maeneo yenu ya kazi, na kwa upande wa Madereva, kuhakikisha mnakuwa na
nakala za Mikataba yenu mnapokuwa katika kazi zenu ili iwe rahisi kwa
Wakaguzi kuiona.
Aidha, ninapenda kuwaarifu kuwa Zoezi la Ukaguzi wa Mikataba ya ajira na
Utekelezaji wa Sheria kwa ujumla litakuwa endelevu na litaendelea pia katika
Sekta nyingine hapa nchini.
Mwisho, ninapenda kutoa wito kwa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji,
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva pamoja na Madereva wote
nchini kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wakaguzi wakati wote wa utekelezaji
wa zoezi hili ili kutoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi kwa namna yoyote ile.