SHIRIKISHO la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Kibaha,mkoani Pwani ,limetoa rai kwa Halmashauri ya Mji huo,kuweka miundombinu rafiki na kuondoa unyanyapaa wakati wa kupiga kura pamoja na kujitokeza kugombea, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 .
Anasema, kwa kuondoa changamoto hizo itasaidia makundi yote kushiriki bila vikwazo nyakati za chaguzi.
Katibu wa shirikisho hilo ,Wilayani Kibaha, Happiness Matagi ,alitoa maoni hayo wakati wa kikao cha wadau wa uchaguzi wa serikali za mitaa,mjini Kibaha .
Alisema, uchaguzi uliopita walishuhudia mazingira yasiyo rafiki kwao ,katika zoezi la upigaji kura kwani maeneo mengine yalikuwa ya ngazi, ukosefu wa msaada kwa wenye ulemavu wa macho na wasiosikia hali iliyosababisha kushindwa kushiriki vema kwenye zoezi hilo.
“Elimu itolewe ili tushiriki na kuthubutu kugombea na tunataka tusinyanyapaliwe kwakuwa na sisi tuna haki ya kuchangamana na wengine katika masuala ya maendeleo na ngazi ya maamuzi”alisisitiza Happiness.
Awali kaimu ofisa uchaguzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Saidi Kayangu alisema ,wamejipanga kuweka mazingira rafiki na kusimamia haki kwa makundi yote ili kuondoa vikwazo wakati wa uchaguzi.
Alifafanua,kwa kutambua hilo ndio maana hatua hii ya awali wameshirikisha asasi mbalimbali, wanawake,vijana ,walemavu na vyama vya siasa kwenye kikao cha wadau ili kupata maoni yao na kwenda kuyafanyia kazi.
Katika hatua nyingine ,Kayangu alihimiza wananchi kujiorodhesha kwenye rejesta za wakazi katika mitaa yote 73 ili kupata takwimu kwa uhalisia hasa idadi ya kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea,:”hatua hii anaelezea itasaidia maandalizi ya uchaguzi kama vile idadi ya karatasi za kupiga kura.
Nae mkurugenzi mtendaji wa asasi ya ushirikiano wa maendeleo ya vijana (YPC) Kibaha,Islael Ilunde aliwaasa vijana na wenye ulemavu kutumia haki yao ya kujitokeza kupiga kura na kugombea.
Pia aliiomba jamii kuwa wakali, kukataa rushwa na badala yake wakati ukifika achaguliwe kiongozi bora na sio bora kiongozi.