Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa ndugu Jimson Mhagama akizungumza na wanufaika wa vikundi vilivyopatiwa mikopo hivi karibuni Ofisini kwake, ikiwa niasilimia kumi ya mapato ya ndani ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.Picha na( Ofisi ya ded Nyasa)
……………
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imetoa shilingi milioni thelathini na tano laki saba themanini na sita elfu mia nne tisini na mbili (35,786,492/=) kukopesha vikundi kumi na mbili (12) vya wanawake, vijana na walemavu ikiwa ni asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akiongea na wanufaika wa mikopo hiyo ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa, Ndugu Jimson Mhagama amewataka wana vikundi hao kuzitumia fedha hizo vizuri kwa kuboresha shughuli mbali mbali za kiuchumi ili waweze kuzirudisha kwa wakati na ziendelee kukopeshwa kwa vikundi vingine vya ujasiriamali na kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.
Mhagama alifafanua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019, imetenga bajeti ya shilingi 42,081,692/= kwa ajili ya kukopesha vikundi vya kina mama, vijana na walemavu ikiwa ni asilimia kumi ya mapato ya ndani kama ilivyoagizwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Tawala za Serikali za Mitaa kupitia Tangazo la Serikali Namba 286 la tarehe 5/4/2019 ambayo imeainisha utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Serikali za Mitaa ambapo inazitaka Halmashauri zote kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani kuwezesha vikundi hivyo.
“Wilaya ya Nyasa tumefanikiwa kuto fedha zote tulizoweka kwenye Bajeti ya mwaka huu wa Fedha na tayari tumesha waingizia kwenye akaunti zenu za vikundi. Nawakumbusha Fedha hizi sio Ruzuku, huu ni mkopo na zinatakiwa kurudishwa ili na vikundi vingine viweze kunufaika na fedha mtakazorudisha”, alisema Mkurugenzi huyo.
Alivitaja Vikundi vya wanawake vilivyopewa mikopo hiyo kuwa ni, Amani (Kata ya Chiwanda), Chakula barafu (Kata ya Mbamba-bay), Umoja Group (Kata ya Mpepo), Acha Tuanze (Kata ya Lumeme), Umoja (Kata ya Kihagara) na Upendo Kiwono (Kata ya Mpepo).
Vikundi vingine ni vya vijana wa Kisasa (Kata ya Luhangarasi), Pikipiki (Kata ya Tingi), Tuungane Pamoja (Kata ya Liwundi), Dhahabu Kijani (Kata ya Mipotopoto) na Kikuso (Kata ya Mpepo) na kikundi kimoja cha walemavu cha Tuthaminiwe kutoka Kata ya Lipingo wilayani hapa.
Aidha alisema kila kikundi kimekopeshwa Tsh milioni tatu (3,000,000/=), kwa vikundi vya kina mama na vijana na kikundi cha walemavu kimekopeshwa shilingi 2,786,492/= (milioni mbili laki saba themanini na sita elfu mia nne tisini na mbili), ambayo watarudisha bila riba kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aliongeza kuwa tayari Halmashauri kwa kipindi cha robo ya kwanza imetoa shilingi 6,295,200/= kwa ajili ya vikundi vitatu vya Mamanilee, Upendo na Muongozo cha vijana wa Kata ya Lipingo.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, Mwenyekiti wa kikundi cha pikipiki kutoka Kata ya Tingi, walisema wanaipongeza sana Serikali kwa kuwajali makundi maalum hasa ya vijana kina mama na watu wenye Ulemavu kwa kuwa makundi hayo ndio hasa yanayo shughulika na utafutaji mitaji kwa kuwa Serikali imewapa mitaji hawata iangusha kwa kuwa watalipa kwa wakati kukuza uchumi katika jamii.
“Nachukua fursa hii kukupongeza sana Mkurugenzi wetu kwa kutupatia mikopo hii kwa kuwa makundi haya ndiyo haswa tunaohangaika kutafuta mitaji na hakuna mwaka ambao Halmashauri hii imetoa mikopo kwa vikundi kumi na tano, hayo ni maajabu. Sisi wanufaika hatuta kuangusha, tutafanya biashara vizuri na tutarudisha kwa wakati ili vukundi vingine vipewe mikopo hii isiyo na Riba”.
Aliongeza kuwa tayari Halmashauri kwa kipindi cha robo ya kwanza ilishatoa shilingi 6,295,200/= kwa ajili ya Vikundi vitatu vya Mamanilee, Upendo na Muongozo cha vijana wa Kata ya Lipingo.