Jengo la Zahanati ya Kikonko katika halmashauri ya Mpimbwe
Dkt. Omary Sukari aliyesimama katikati akitoa elimu ya matumizi ya vyandarua kuzuia malaria kwa wanawake wajawazito katika zahanati ya Mnyamasi halmashauri ya Nsimbo
Kinamama na watoto wao wakisubiri huduma za matibabu katika zahanati ya Kikonko
…………………………
Na Mwandishi Wetu Katavi
Mkoa wa Katavi umechukua mkakati wa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kupitia kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa kinamama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano
Mkakati huo umetangazwa na mratibu wa malaria Mkoa wa katavi bwana Stephano Kahindi ambaye amesema mkoa umetenga kiasi cha shilingi milioni hamsini na tano kwa ajili ya kununua viuatilifu vya kunyunyiza katika madimbwi kwa ajili ya kuua viluwiluwi wanaosababisha ugonjwa wa malaria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na ofisi ya takwimu taifa juu ya viashiria vya ugonjwa wa malaria mkoa wa katavi una maambukizi kwa asilimia 7.1
Dkt Omary Sukari ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, akiwa katika zahanati ya Mnyamasi katika halmashauri ya Nsimbo wilaya ya Mpanda alipata fursa ya kuzungumza na wanawake wajawazito ambapo aliwapa elimu juu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa
Aidha Dkt. Sukari aliwaasa wananchi juu ya matumizi mabovu ya vyandarua hivyo kwani baadhi ya wananchi wamekuwa wakivitumia kuvulia samaki na kufugia kuku
Alisema ugonjwa wa malaria unapompata mtoto na kushindwa kutibiwa mapema unaweza kuathiri afya ya ubongo wa mtoto
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Dkt Sebastian Siwale kufuatia halmashauri hiyo kuwa karibu na Hifadhi za wanyama pori pamoja na kuwepo kwa chemchem nyingi za maji; hali hiyo inapelekea maeneo mengi kuzungukwa na maji na majani na hivyo kusababisha mazalio ya mbu waenezao ugonjwa wa malaria kuzaliana kwa wingi
Ameongeza kuwa hali hiyo inachangia ongezeko la wagonjwa wa malaria hasa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kutokana na halmashauri kushindwa kuwadhibiti mbu hao
“Katika watoto wanaoletwa katika vituo kupimwa kati ya watoto kumi”, watoto saba hadi nane wanakutwa na malaria, alisema Dkt Siwale
Pia ametoa wito kwa wananchi kujitahidi kusafisha maeneo yao kwa kuchoma nyasi na kufukia madimbwi ya maji ili kuzuia mazalia ya mbu