Baadhi ya vifaa vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 vilivyotolewa kwa Taasisi ya Uvuvi nchini (TAFIRI) kwa ajili ya kuendeleza tafiti za sekta ya uvuvi nchini
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (mstari wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika hatua za mwisho za mafunzo kabla ya mafunzo hayo kuhitimishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah.
****************
Na. Edward Kondela
Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema wizara hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) imeweka mikakati ya kufanya tafiti ikiwa ni moja ya vipaumbele katika kukuza sekta ya uvuvi nchini katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyokuwa yakiendeshwa kwenye makao makuu ya TAFIRI, Dkt. Tamatamah amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia Sino-Africa Joint Research Centre (SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) kwa kushirikiana na TAFIRI yana lenga kuhakikisha washiriki wa mafunzo hayo ya siku sita ya uelewa wa ufuatiliaji wa ubora na unadhifu wa maji na mazingira, wanafanya tafiti ili kuleta matokeo chanya katika ukanda wa Bahari ya Hindi, maziwa na mito iliyopo nchini.
Dkt. Tamatamah amesema pia washiriki wamepata mafunzo kupitia mihadhara iliyotolewa na wakufunzi wabobezi kutoka China na Tanzania pamoja na kukusanya takwimu kutoka katika mito iliyopo Mkoani Dar es Salaam na kuchakata takwimu hizo katika maabara ya TAFIRI.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAFIRI Dkt. Semvua Mzighani amesema kupitia mafunzo hayo Serikali ya Watu wa China, SAJOREC na EAGLU wametoa vifaa vya utafiti vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 ambavyo vitatumika kwa tafiti za kuangalia ubora na unadhifu wa maji na mazingira kwa ujumla.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuwafundisha wenzao katika sekta ya uvuvi ili kuhakikisha viumbe vinavyotegemea maji katika maisha yao ya kila siku, vinapata maji safi na salama kutokana na tafiti zitakazokuwa zikifanywa na kutafuta njia mbadala za kuhakikisha maji yanaendelea kuwa salama na kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi kuathiri usalama wa maji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo yatawezesha taasisi mbalimbali zinazohusika na usalama wa maji kufanya tafiti zenye matokeo chanya ili maji ya Bahari ya Hindi, maziwa na mito katika Ukanda wa Afrika kuwa salama na kupata suluhu namna ya kukabiliana na mabadiliko yoyote ya tabia nchi ambayo yanaweza kusababisha athari katika maji hayo.
Mafunzo hayo yameshirikisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Ethiopia pia walikuwepo waendesha mafunzo hayo kutoka China.