Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Injinia Deusdedit Kakoko akizungumzia mafanikio na miradi ya Mamlaka hiyo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Bandari jijini Dar es salaam jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Injinia Deusdedit Kakoko akisikiliza baadhi ya maswali ya waandishi wa habari katika mkutano huo.
………………………………………………….
MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), inatenga kiasi cha shilingi bilioni 400 mpaka 500 kwa mwaka ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya Bandari za bahari kuu pamoja na Maziwa Makuu
Mkurugenzi wa (TPA), Injinia Deusdedit Kakoko ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana na kusema kwamba TPA inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Kuongeza kina katika Bandari ya Tanga na gati zingine mbili ambapo jumla ya shilingi Bilioni 2 zitatumika.
Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine tunanunua pia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo kwenye meli na tunafanya hivyo katika bandari mbalimbali za Bahari Kuu pamoja na Maziwa Makuu.
Kumekuwepo na ujenzi wa bandari mbalimbali, Ujenzi wa Meli mpya pamoja na ukarabati wa meli za zamani na ununuzi wa mitambo mbalimbali ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa katika bandari zetu.
Miradi hiyo inaendelea katika bandari za Dar es salaam, Tanga, Mtwara, kwenye bahari kuu, Pia inaendelea kwenye Maziwa Makuu yote zikiwemo Nyamirembe Geita, Bukoba, Kemondo, Musoma na zingine nyingi.
Ameongeza kuwa Bandari zingine za ziwa Tanganyika ni Kigoma yenyewe, Karema , Kabwe, Kipiri, Kasanga na ziwa Nyasa kuna mradi kubwa wa ujenzi wa meli ya Abiria na mizigo MV Mbeya II ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba pamoja na ujenzi wa bandari ya Ndundu kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe ambapo pia meli mbili za mizigo MV Njombe na MV Ruvuma zimekamilika na zinafanya kazi.
Akizungumzia makusanyo ya Mapato katika bandari amesema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 818 mwaka 2017/18 hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 900 mwaka 2018/19 ambapo ongezeko hilo ni zaidi ya Sh. bilioni 90 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Mapato yatokanayo na bandari yameongezeka kwa zaidi ya Sh. bilioni 90 ingawa bado hatujafunga hesabu hadi leo (jana), kutoka Sh. bilioni 818 mwaka 2017/18 hadi Sh. bilioni 900 ambazo tumeshakusanya hadi sasa na tunaamini tukifunga hesabu yatakuwa yameongezeka,” amesema Kakoko
Aidha, amesema katika mwaka huu wa fedha uliomalizika leo, wanatarajia kutoa Mrabaha Serikalini wa zaidi ya Sh. bilioni 200.
“Tunatarajia kutoa mrabaha kwa Serikali si chini ya bilioni 200 ambazo ni nje ya kodi ya taasisi nyingine za umma na halmashauri zetu na mwaka jana tuliongoza naamini na mwaka huu tutaongoza,” amesema Kakoko.