**************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
WAZIRI Wa Viwanda na Biashara ,Innocent Bashungwa amekemea baadhi ya Watanzania wanaopotosha na kukandia kuwa korosho ya Tanzania iliyopo kwenye maghala ,haina ubora ambapo amewapasha kuacha propaganda zisizo na tija kwa Taifa.
Aidha ameielekeza DAWASA na TANESCO kukimbilia fursa ya kutoa huduma ya maji na umeme kwa wawekezaji pasipo kuwakwamisha huduma hizi ili wazalishe zaidi na serikali ipate mapato makubwa.
Akitembelea kiwanda cha korosho Terra cashew kilichopo ,Tanita wilayani Kibaha mkoani Pwani, Bashungwa alieleza watu hao hawalitakii mema Taifa.
Aliweka bayana kwamba, tayari kwa sasa kuna korosho ya kutosha na yenye ubora katika maghala 37 nchini .
“Nchi yetu inategemea zao hili la kibiashara wakitokea watu wapotoshaji inakuwa haileti maana na kushusha sifa ya nchi katika biashara ya zao hilo”.
“Nilitembelea maghala hayo na wataalamu wangu, tumejiridhisha ,korosho yetu ni nzuri kwa grade ya I na ya II na ipo katika thamani”alisisitiza Bashungwa.
Akizungumzia suala la ubanguaji korosho ,Bashungwa alibainisha ,watu wanapata ajira katika ubanguaji na kukuza pato la Taifa,kuelekea katika uchumi wa kati.
Alisisitiza ubanguaji wa viwango na ubora kwa wakati ili kuwa na korosho yenye ubora.
Wakati huo huo ,Bashungwa alitembelea kiwanda cha KEDS ambacho kinazalisha soft care (pempas) na sabuni za unga na kutajiwa changamoto ya upungufu wa umeme na maji ya uhakika.
“Endapo wakibaniwa huduma hizi uzalishaji unapungua tuvutie wawekezaji,hii ni biashara sio kama tunawapa msaaada mjue kama hawa hawazalishi basi na serikali inakosa mapato” .
Nae mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka alisema, mpango uliowekwa na serikali kwenye maghala na kuhakikisha wakulima hawapunjwi ni mpango mzuri kwa maslahi ya wakulima na Taifa.
Koka alieleza ,hao wanaopotosha juu ya korosho iliyopo kwenye maghala zimeoza na kuharibika wapuuzwe.
Awali Ofisa Utawala wa Terra Cashew ,Peter Christopher alitaja changamoto zinazowakabili ni ucheleweshaji wa kutolewa makontena ya mitambo na vipuri bandarini kwa takriban miezi mitatu na zaidi.
Pia tatizo likiwa kupewa taarifa zisizo kamilika mara kwa mara kuhusu nyaraka wanazozihitaji .
Peter alisema kwa sasa kiwanda hicho kina ajira rasmi 120 na ajira zisizo rasmi 300.