Mwanariadha Damian Christian wa Arusha (mbele) akiwaongoza wenzake Robert Francis wa Singida aliyeshika nafasi ya pili na Hoja Samwel wa Simiyu wakichuana vikali katika mbio za mita 1500.
Salma Ismail (392) kutoka Mwanza ambaye alishinda mbio za mita 1500 wasichana akiwa mbele ya wenzake Valaria charles (569) wa Singida ambaye alishika nafasi ya pili na Grace Mpina (080) kutoka Geita ambaye alishika nafasi ya tatu mara baada ya kumaliza mbio hizo leo asubuhi.
Washiriki wa mchezo wa riadha fainali maalum za UMITASHUMTA wakikimbia mbio za mita 100 leo katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara
*****************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Wanariadha Damian Christian kutoka mkoa wa Arusha na Salma Ismail wa Mwanza wameshinda medali za dhahabu kwa wavulana na wasichana kwenye fainali za mbio za mita 1500 zilizofanyika leo katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
Damian alitumia dakika 4:16:47 kumaliza mbio hizo huku akifuatiwa kwa karibu na Mwanariadha Robert Francis kutoka Singida ambaye alitumia muda wa dakika 4:17:00, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Hoja Samwel wa Simiyu ambaye alitumia dakika 4:19:88.
Kutokana na matokeo hayo Damian amejinyakulia medali ya dhahabu, Robert atapata medali ya fedha ambapo Hoja atapata medali ya shaba.
Kwa upande wa wasichana medali ya dhahabu imechukuliwa na mwanariadha Salma Ismail wa Mwanza ambaye alikimbia kwa muda wa dakika 4:46:65, ambapo medali ya fedha ilichukuliwa na mwanariadha Valaria Charles wa Singida ambaye alishika nafasi ya pili baada ya kutumia muda wa dakika 4:47:15 huku medali ya shaba ilikwenda kwa mwanariadha Grace Mpina wa Geita aliyetumia muda wa dakika 4:47:25.
Katika mashindano ya kuruka juu ambayo yalifanyika leo katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara wanariadha watatu wa kutoka mikoa ya Mara, Kilimanjaro na Geita wamejinyakulia medali za dhahabu, fedha na shaba.
Nafasi ya kwanza ilishikwa na Mwanariadha Yunus Chacha Mondera wa Mara ambaye aliruka urefu wa mita 1 na sentimita 38, nafasi ya pili imechukuliwa na mwanariadha Witness Martin kutoka Kilimanjaro ambaye aliruka urefu wa mita 1 na sentimita 37, huku nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mectrida Kasandhao wa Geita. Matokeo hayo yamewawezesha wanariadha Yunus, Witnes na Mectrida kujinyakulia medali za dhahabu, fedha na shaba.