Kazi siku hii nayo ikaisha nikarudi hotelini pamoja na wenzangu ili kumalizia kazi za siku hiyo na kujiandaa na safari ya Musoma mkoani mara ili kuona nini kinaendelea kuhusu wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya bandari katika maziwa makuu nchini.
Basi asubuhi kulipokucha Juni 4 tuliamka mapema kabisa Dereva Hassan Shaban akaja akatuchukua huku tukiwapitia waandishi wenyeji wa Mwanza Mabere Makubi wa ITV na Jonathan Mussa wa Mwananchi tukaanza safari ya Musoma.
Tulikwenda huku tukipiga story na kubadilishana mawazo ya hapa na pale, Basi tukiwa tunapita kandokando ya mbuga ya wanyama ya Serengeti tuliona wanyama wengi miongoni mwao walikuwa Nyumbu watu wakawapa majina kibao huku tukaendelea na safari, mapema kabisa tuliingia Musoma moja kwa moja tukaenda Bandarini.
Hapa tulikuta Bandari ya Musoma inaendelea na shughuli zake kwa kupokea na kusafirisha mizigo ya kutosha kabisa tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo bandari hiyo ilikuwa imesimamisha kazi hizo.
Hapa tukazungumza na mmoja wa wafanyabiashara Bw. Justine Rukaka Mwakilishi wa kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula kwa mbegu za Pamba cha Mount Meru Millers ambaye aliishukuru Mamlaka ya Bandari Ziwa Victoria kwa kurejesha huduma za usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Musoma
Alisema huduma hii imewaondolea adha ya gharama kubwa za kusafirisha malighafi ya kutumia kiwandani hapo ambazo kwa sasa zimepungua kwa kiwango kikubwa baada ya huduma hiyo kurejeshwa.
“Tumekuwa tukipokea tani 250 mpaka tani 500 za mbegu za Pamba kwa mara moja kulingana na ukubwa wa meli inayoleta mzigo siku hiyo kutoka nchini Uganda, hivyo kwetu sisi imekuwa rahisi kwa uendeshaji na uzalishaji wa bidhaa kutokana na gharama za usifiri kupungua”. Alisema Bw. Lucas Lukaka.
Kwa upande wa Almachius Vedasto Rwehumbiza Msimamizi wa Bandari ya Musoma alisema Bandari hiyo inao uwezo wa kupokea meli tatu kwa wakati mmoja zenye tani 1,500 mpaka 5,000.
Tulipotoka hapo tukaelekea upande wa pili wa bandari ili kushuhudia Ujenzi wa Gati la Mwigobero katika bandari ya Musoma ambao tayari umekamilika na limeanza kutumika, Gati hilo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 605,036,150.00.
Vyombo mbalimbali vya usafiri wa majini hasa vya abiria, Wavuvi vitatia nanga hapo kupakia au kushusha abiria na mizigo mbalimbali hivyo kurahisisha shughuli mbalimbali za kibiashara kati ya miji, Visiwa na vijiji vilivyomo kandokando ya ziwa victoria.
Hizi zote ni juhudi Mahsusi za Mh. Rais wa Jahuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali wanaoishi katika visiwa, Miji au Vijiji vilivyopo kandokando ya Maziwa yetu makuu wanapata huduma ya usafiri na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, Kufanya biashara na huduma zingine ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
UTORO WA MABERE MAKUBI WA ITV (Wenyewe tulikuwa tukimtania Memeee ne……)
Hapa ngoja nizungumzie kidogo utoro wa Kaka Mabere Makubi. Mabere Makubi kidogo alikuwa ananishangaza manake alikuwa anatoroka sana eneo la tukio hasa tukimaliza vitu muhimu, Lakini Baadae nilipomuelewa lengo lake nilijifunza kitu kutoka kwake.
Tulipomaliza kazi katika bandari ya Mwigobero Musoma tukawa tunajiandaa kuingia kwenye gari ili tuanze safari ya kurudi Mwanza lakini kila tukimuangalia Mabere Makubi haonekani, Tukajaribu kuangalia huku na kule hatukumuona, Kumbe alikuwa ameenda eneo la pembeni kidogo amejichanganya na wananchi akipiga picha za video na kufanya mahojiano na baadhi ya watu.
Hii ikawa ndiyo tabia yake kila wakati anaweza kuwa wa kwanza kushuka kwenye gari au wa pili au akawa hata wa nne, lakini kurudi tena kupanda gari baada ya kumaliza kazi anakuwa mtu wa mwisho.
Mara nyingi tulikuwa tunakaa kiti kimoja (Vijana wakituita eti Wazee) basi siku moja nikamuuliza, Kwanini unakuwa mtu wa mwisho kupanda gari kaka? Mabere Makubi akanijibu hivi “Unajua kaka kazi yetu watu wa TV ni ngumu ili habari iwe nzito na iliyokamilika lazima uwe na vyanzo vya habari angalau viwili au vitatu hapo mambo yatakuwa mazuri.
“Sababu nyingine ni kwamba watazamaji wa Luninga mara nyingi pamoja na kusikiliza ujumbe wa habari yenyewe wanapenda sana kuangalia picha mbalimbali zinazotembea wakati taarifa ya habari yako ikiendelea, Chanzo kimoja tu cha habari hiyo itakuwa bado haijakamilika.
Ndiyo maana utaniona mara kwa mara nahangaika ili kupata picha (Cuts) zenye vionjo tofauti, Lakini pia ukiwahoji watu zaidi ya mmoja au wawili kila mtu atakuambia alichoshuhudia na anachokielewa kuhusu habari yenyewe na hii ndiyo ladha ya habari Brother.” Nikamuelewa sana Mabere Makubi.
Hii ilinipa kitu yaani kufanya kazi kila siku na kufanya kwa pamoja na watu wenye uelewa na uzoefu mbalimbalivijana kwa wazee kunatujenga kuwa wajuzi wa kazi zetu kila tunapoona jambo tofauti au jipya na kutupa uzoefu zidi ya kile unachokifahamu ila sijui kama vijana wangu Hirraly na Willy walikuwa wameshtukia hii kwamba pamoja na kazi wako darasani pia.
Basi tulirejea jijini Mwanza kuendelea na uchakataji wa habari ili kuwa ziwe tayari kwa kutumika kwenye vyombo vyetu siku hii ikawa imeisha.
Ratiba ya siku iliyokuwa inafuata Juni 5 ilikuwa ni safari ya kwenda Sengerema ambako wananchi wa Lushamba hawakuwa na bandari tangu mwaka 1958 sasa wamejengewa baada ya miaka 61 kupita, Je? wananchi wanasemaje kuhusu Rais Dkt. John Pombe Magufuli……………………………. INAENDELEA
ENDELEA KUFUATILIA SIMULIZI HII NITAKUSIMULIA MAAJABU YA RAIS MAGUFULI NILIYOYAONA.