Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
TIMU ya Mtibwa Sugar imetetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya kuwafunga wenyeji Azam FC kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Kipa Hatibu Waziri alitokea benchi dakika ya 119 kwenda kumalizia hatua ya matuta, akapangua mkwaju wa nne baada ya Azam kukosa tuta moja awali na Mtibwa wakatwaa tena taji hilo baada ya mwaka jana kufanya hivyo Dodoma.
Awali, Yanga SC ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu katika michuano hiyo baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu wao, Simba SC, mabao ya Kilaza Mazoea dakika ya 35 na Julius Wilson Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
Samwel Jackson wa Azam FC alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mashindano, Onesmo Mayaya Mfungaji Bora kwa mabao yake matano, Razack Ramadhan wa wote wa Mtibwa Sugar akawa Kipa Bora, Kocha Bora Said Maulid Kalikula ‘SMG’ wa Yanga SC na Refa Bora ni Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam.