JUMLA ya walengwa 30,893 wamenufaika na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III)mkoani Pwani, huku zaidi ya sh.bilioni 29 zikiwa zimepokelewa kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi Jan 2019.
Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha mwaka 2018 -2019, katika kikao cha kutathmini shughuli za utekelezaji wa mpango huo, mratibu wa TASAF Mkoani hapo,Asha Itelewe amesema mpango huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa walengwa.
“Wameweza kubadili maisha yao kwani wapo ambao walikuwa wakiishi kwenye nyumba za makuti na sasa wameezeka kuwa na nyumba bora zenye mabati “Maudhurio ya watoto wa kaya hizo mashuleni yamekuwa mazuri na mlo wa chakula imeongezeka kutoka mlo mmoja hadi milo mitatu kwa siku.
Itelewe anaongeza ,asilimia 70 ya walengwa wameweza kuanzisha miradi ya kilimo na mifugo na asilimia 50 wameanzisha vikundi vya kiuchumi ili kujiinua kimaendeleo.
Licha ya mafanikio hayo ,Itelewe anataja changamoto zinazowakabili ni upungufu wa raslimali fedha na walengwa kushindwa kujiunga na bima ta afya kutokana na kiwango cha kujiunga kupanda kutoka 10,000 hadi 30,000 hivyo wengi wao kushindwa kumudu kiasi hicho.
Nae mratibu wa mpango wa kunusuru kaya maskini wilaya ya Mkuranga Safina Msemo,alielezea wameanzisha kikundi kilichojiwekea mkakati wa kuanzisha kilimo cha mapapai .
Msemo anabainisha mkakati mwingine ni mradi wa chaki ambapo wameongea na wilaya kuomba endapo wataanza rasmi basi shule za serikali zinunue chaki kwa kikundi hicho.
“Mradi huu tumeona unamanufaa na nimeshaulizia gharama za mashine ni zaidi ya milioni mbili na nimeongea na baadhi ya wadau ambao watanisaidia kununua mashine hiyo”alisema Msemo.
Awali akifungua kikao hicho,katibu tawala wa mkoa wa Pwani,Theresia Mbando anasisitiza suala zima la uwajibikaji ,uadilifu na ubunifu wa hali ya juu kuwatumikia walengwa na kuwatolea ufafanuzi wa kero zao na kama kuna madai yao yashughulikiwe kwa wakati.