Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi. Nuru Mwasulama akitoa taarifa fupi ya uanzishwaji wa Kanda hiyo itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na makao makuu yake yakiwa Bariadi Mjini, katika uzinduzi waa kanda hiyo uliofanyika Juni 20, 2019 Mjini Bariadi.
Kaimu Mganga mkuu wa Mkoa, Dkt. Mugune Maeka akitoa neno la shukrani mra baada ya kuhitishwa kwa uzinduzi wa Kanda ya Ziwa Mashariki ya Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga, Juni 20, 2019 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (katikati mbele) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi, wataalam wa mkoa wa Simiyu na Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) mara baada ya Uzinduzi wa Ofisi ya Mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa Mashariki itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na makao makuu yake yakiwa Bariadi Mjini, Uzinduzi umefanyika Juni 20, 2019 Mjini Bariadi.
………………….
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imefungua rasmi Ofisi ya Kanda mpya ya Ziwa Mashariki itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ambapo makao makuu ya kanda hiyo yatakuwa Mjini Bariadi mkoani Simiyu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi. Nuru Mwasulama amesema mamlaka hiyo imeanzisha Kanda Mpya ya Ziwa Mashariki inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ili kusogeza huduma kwa wananchi na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Amesema ofisi hii itajishughulisha na usajili wa maeneo yanayo jihusisha na uzalishaji na uuzaji wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, kupokea maombi ya usajili wa bidhaa za vyakula vinavyofungashwa, kufanya ukaguzi wa bidhaa za vyakula katika soko kuwalinda walaji na kudhibiti usindikaji wa chakula dawa na vipodozi.
Kazi nyingine zitakazofanywa na kanda hii ni kutoa vibali vya uingizaji nchini na usafirishaji wa chakula nje ya nchi, kufanya ufuatiliaji wa bidhaa za vyakula katika soko, kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa, vipodozi na vifaa tiba pamoja na kuelimisha na kutoa taarifa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuhusu bidhaa zinazothibitiwa na mamlaka.
Aidha, Mwasulama amesema Ofisi ya kanda hii itatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambapo wataalam waliopo kwenye wilaya, manispaa, miji na majiji watasimamia sheria ya chakula na dawa kwa mujibu wa kanuni ya kukasimu baadhi ya majukumu na madaraka ya TFDA katika Halmashauri.
Akizungumza na baadhi ya wataalam wa Mkoa wa Simiyu na TFDA katika ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema Taasisi nyingine zinazohitajika katika uwekezaji wa viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji zikaiga mfano wa TFDA kwa kusogeza huduma karibu na wananchi ili waweze kupata huduma kwa wakati.
“Hiki kilichofanywa na TFDA ni vizuri taasisi nyingine nazo ziige, kama leo TFDA ipo Simiyu kama Kanda ya Ziwa Mashariki ningetamani kuwaona TBS, NEMC, OSHA wako Simiyu kama Kanda ya Ziwa Mashariki na Taasisi zote ambazo kwenye uwekezaji wa viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji zinakuwa karibu na maeneo ya kutolea huduma” alisisitiza Mtaka.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaotekeleza majukumu waliyokasimiwa na TFDA kufanya majukumu hayo kwa mujibu sheria huku akiwaasa kuacha tabia ya kufungia biashara za wananchi bila kuwaelimisha badala yake wawasaidie kuwapa elimu ili wazalishe bidhaa bora kwa walaji.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Dkt. Mike Mabimbi akizungumza kwa niaba ya waganga wakuu wa wilaya ambao ni Makatibu wa kamati za ukaguzi wa chakula na dawa amesema watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa majukumu wanayokasimiwa na TFDA kwa mujibu wa sheria na akashukuru TFDA kusogeza huduma karibu na wananchi.