Wakulima wakipata elimu matumizi sahihi ya mizani Geita
Baadhi ya wakulima wa Pamba wakiendelea kupatiwa elimu ya matumizi ya mizani ambazo zimekaguliwa na kuhakikiwa na wakala wa Vipimo WMA mkoa wa Geita.
***********************
Wakala wa Vipimo WMA wamewahasa wakulima wa pamba kuhakikisha mizani ambazo hutumia katika kupima zao hilo imekaguliwa na kubandikwa stika pamoja na seal inayoonesha nembo ya bibi na bwana na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika.
WMA wameweza kufika katika mkoa wa Geita na kutoa elimu hiyo kwa wakulima wa pamba ili kuwepo na matumizi sahihi ya mizani katika ununuzi wa pamba.
Akizungumza na wakulima hao Meneja wa WMA Mkoa wa Geita Bw. Zakaria Kisamo amewaambia wakulima kwamba wanatakiwa kumpatia ushirikiano wa kutosha Afisa Vipimo kwa kumsaidia kumpa taarifa zote atakazozihitaji, kupeleka mazao yake kuuza katika soko au kituokilichoteuliwa na kukubalika na bodi ya pamba na kuhakikisha anauza pamba yake kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na wakala wa vipimo.
“Muuzaji hakikisha mizani inasoma (0) kabla ya kuweka mzigo, pia ukishusha mzigo wako angalia kama mizani inasoma (0)kama haisomi sufuri wakati haina mzigo . anza upya kufuata mtiririko wa hapo juu kabla ya kupima” Amesema Bw. Kisamo.
Pamoja na hayo Bw. Kisamo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuuza na kununua pamba kwa kutumia mizani iliyo hakikiwa na wakala wa vipimo ikiwemo mkulima atapata fedha kulingana na thamani ya mazao yake pamoja na kufanya biashara ya haki na kuepuka migogoro ambayo imekuwa ikizoeleka katika biashara na vilevile kama kijiji kimeshanunua jiwe la kilo20, unatakiwa kuweka kwanza jiwe hilo ili kujihakikishia Zaidi usahihi wa mizani hiyo kwani mizani itasoma 20.0.
“Afisa wa Vipimo anatakiwa kujitambulisha kwa uongozi wa mtaa pamoja na kuonesha kitambulisho chake cha kazi muda wowote kitakapohitajika”. Ameongeza Bw. Kisamo.