Home Mchanganyiko SERIKALI YAOKOA MABILIONI UENDESHAJI MASHAURI YA MADAI

SERIKALI YAOKOA MABILIONI UENDESHAJI MASHAURI YA MADAI

0

****************************

Serikali imesema mabadiliko kwenye sekta ya sheria nchini hususani Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu yameanza kuleta tija baada ya kuongeza ufanisi na
kuokoa fedha ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kuwalipa mawakili
binafsi.

Akijibu swali la Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kuebenea ambae
alitaka kujua kiasi cha fedha ambacho serikali imeokoa tangu maboresho
kwenye sekta hiyo yaanze kutekelezwa, ambapo pamoja na mambo
mengine yalianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo imepewa
mamlaka ya kusimamia, kuendesha na kuratibu mashauri yote ya madai
kwa niaba ya Serikali nchini.

Kwenye majibu yake Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga
alimueleza mbunge hyo kuwa kwenye Mwaka wa Fedha 2018/19 pekee
Serikali imeweza kuokoa zadi ya shilingi bilioni tisa (9,018,957,011),
ambazo kama sio maboresho kwenye sekta hiyo zingetumika kulipa
makampuni binafsi ya uwakili.

Aidha, Dkt. Mahiga aliendelea kulieleza Bunge kuwa Serikali itaendelea
kutumia Mawakili binafsi kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pale itakapothibitika kuwa ni lazima kufanya hivyo. Alitoa mfano wa
vigezo vinavyotumika kutumia mawakili binafsi ni shauri kufunguliwa
kwenye mahakama ambazo sio za kimataifa na sheria za nchi husika
haziruhusu uwakilishi wa mwanasheria kutoka nje ya nchi hiyo.

Kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa Dkt. Mahiga ameliambia bunge
kuwa uendeshaji wa mashauri hayo utendelea kuishirikisha Ofisi ya Wakili

Mkuu wa Serikali kwenye kila hatua ya mwenendo wake tofauti na hapo
awali.

Kuhusu baadhi ya mashirika ya umma kuendelea kutumia mawakili
binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi
amelieleza Bunge kuwa mashirika hayo ni yale ambayo mashauri yake
yalianza kabla ya maboresho kwenye sekta hiyo hayajaanza kutekelezwa
na uendeshaji wa mashauri utatekelezwa kwa kushirikiana na Wakili Mkuu
wa Serikali.