Shirika la umeme Nchini TANESCO limetekeleza agizo la rais alilotoa juni 13 Ikulu mara baada ya kukutana na wabunifu wa umeme kutoka mkoani Njombe la kuwataka kuwatembelea , kuwatambua , kuwapa ushauri wa kitalaamu pamoja na fedha mil 15 kila mmoja huku lengo kuu likiwa ni kuthamini na kutambua ubunifu na jitihada ambazo zimechukuliwa na watu hao kitimiza ndoto zao.
Akizungumza mbele ya umati wa wakazi wa kijiji cha Lugenge wakati akikabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya mil 10 pamoja na fedha taslimu mil 5 kwa wabunifu wote wawili akiwemo John Fute maarufu Dr Pwagu na Laniel Ngailo mara baada ya kutembelea vituo hivyo vilivyobuniwa na kienyeji na watu hao mkurugenzi mkuu wa TANESCO Dr Titho Mwinuka amesema serikali itaendelea kuthamini na kutoa usaidizi wa kila hali ili kufikisha ndoto panapo stahili ndoto za wabunifu hao.
Amesema timu hiyo ambayo imetumia siku mbili kutembelea na kukagua kitalaamu vituo hivyo vya kuzalisha umeme vilivyobuniwa kienyeji ambapo amesema katika ziara hiyo timu imejifunza mambo mengi ikiwemo uwepo wa watu wengi wabunifu ambao wanafanya mambo makubwa bila ya kujulikana na kuahidi kuwasaidia wabunifu hao kwa kila namna ili wawe na uwezo wa kuzalisha umeme mwingi zaidi utakanufaisha na vijiji jirani.
“Watalaamu wa shirika wamefanya utafiti na upimaji katika kituo cha Msete cha bwana Pwagu pamoja cha Lugenge na kubaini vituo hivyo vikiboreshwa kisasa vinaweza kuzalisha kiwango kikubwa cha umeme utakaokuwa na manufaa kwa watu wengi alisema Dr Mwinuka”
Kwa upande wao wabunifu hao ambao ni John Fute maarufu Pwagu na Laniel Ngailo ambao ni wabunifu wanasema imekuwa kama ndoto kwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kutambua uvumbuzi na ubunifu wanaoufanya na kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapa watalaamu na fedha ili kuboresha huduma zao huku pia wakionyesha hisia zao juu ya hatua ya TANESCO kuwakabidhi fedha taslimu mil 5 na hundi ya mil 10 kila mmoja kama ambavyo iliahidiwa mbele ya rais Magufuli
Wabunifu hao wamesema awali wakati wameanza kujaribu kubuni miradi yao walikuwa wakidharauriwa na jamii zinazo wazunguka jambo ambalo limekuja kuwa nuru baada ya kutambuliwa na rais hadi kuitwa ikulu kuzungumza nao.
Katika timu iliyofika kwa wabunifu hao ilikuwa ni pamoja na naibu katibu mkuu wa wizara ya maji mhandisi Emmanuel Kalombelo ambae pia ameonyesha kufurahishwa na ubunifu aliouona na kuagiza serikali kuboresha ili kuendana na kasi ya teknolojia karakana ya mzee John Fute maarufu Pwagu ili kiweze kuwa kituo kikuu cha ubunifu katika mkoa wa Njombe na Kanda ya nyanda za juu kusini huku pia akiitaka tume ya sayansi na teknolojia kuhakikisha inawatambua wabunifu kutoka sekta mbalimbali waliopo nchini.
Mara baada ya agizo naibu katibu mkuu ,mratibu wa masuala ya habari na maarifa kutoka COSTECH ndugu Deusdedith Lenard anasema agizo hilo litatekelezwa haraka iwezekanavyo kwa kuanza mara moja uboreshaji wa kiota hicho cha ubunifu kilichopo nyumbani kwa Pwagu ili kiweze kutumiwa na watu wengi kubini vitu mbalimbali.
Ujio wa timu hiyo iliagizwa na rais juni 13 wabunifu walipokutana na rais kujadili masuala mbalimbali kuhusu sekta ya umeme na ubunifu wanaoufanya umewagusa wakazi wa vijiji vya Lugenge na Msete mjini Njombe ambao wanasema wamefurahishwa na kitendo cha rais kutambua uwezo wa ndugu zao na kueleza kuwa uwezo wa umeme huo uliobuniwa kienyeji umekuwa msaada kwao
Timu hiyo imewasili ikiwa na watalaamu kutoka TANESCO, COSTECH,REA, Wizara ya maji,Ewura na Mamlaka za bonde la mto Rufiji na Nyasa huku kila mmoja akitazama namna ya kuwasaidia wabunifu hao ambao wamekumbana na changamoto nyingi mpaka kufikia hapo.