Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akizungumza wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Baadhi ya Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa ibada ya kuwawekea mikono iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Rochester, Uingereza, James Langstaff na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula, wakiwawekea mikono Mashemasi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa wakati wa ibada iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula akizungumza wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemashi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga kabla ya kuanza kwa wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa
***************************
Na. Happiness Shayo
Waumini wa dini ya kikristo nchini wamehimizwa kutoa mchango kwenye
maeneo mbalimbali hususan katika kujenga makanisa, shule na hospitali
ambazo zitatumika kutoa huduma za kijamii kwa ajili ya maendeleo ya
taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika
(Mb) wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa
Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika
kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Mhe. Mkuchika amewataka waumini wa kanisa hilo kuchangia maendeleo
ya kanisa, kwani mafundisho ya kanisa yanawataka waumini kutoa kwa
hiyari ili kuisaidia Serikali kuboresha huduma za kijamii ambazo ndio
chachu ya maendeleo ya taifa.
“Kanisa linatufundisha ni heri kutoa kuliko kupokea kwa kuwa tukitoa
tunapata thawabu kwa Mungu” Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa, Kanisa la Anglikana Tanzania ni
Kanisa la tatu kuwa na wafuasi wengi lakini katika shughuli za maendeleo
limekuwa nyuma sana.
“Kanisa letu limekuwa nyuma katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo
hususan kujenga makanisa mengine, shule na hospitali. Ni lazima
tubadilike kwa sababu Wamissionari wa Kigeni tuliowategemea sasa
hawapo” Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika alihamasisha uchangiaji wa ujenzi wa Kanisa
ambapo takribani milioni nne zilipatikana.
Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Given Gaula amemshukuru Mhe.
Mkuchika kwa kujitoa katika kuhamasisha uchangiaji wa maendeleo ya
kanisa na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta
maendeleo katika Taifa.
“Pamoja na masuala ya kiimani na kiroho, Kanisa la Anglikana limejipanga
kutoa elimu katika jamii kwa kujenga shule ya sekondari na ufundi katika
Wilaya ya Chemba na shule ya awali katika eneo la Bicha” Dkt. Gaula
amesema na kuongeza kuwa, kanisa hilo lina miradi mingine kama mradi
wa hosteli na vikundi vya kijamii vya kujikwamua kiuchumi vinavyojulikana
kama Church Community Mobilization Process.
Ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi imehudhuriwa na
viongozi wa serikali wa wilaya ya Kondoa, washirika wa Kanisa Anglikana
kutoka Marekani, Uingereza na vikundi mbalimbali vya dini kutoka kanisa la
Anglikana Dayosisi ya Dodoma.