NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi(kushoto) akikabidhiwa Tisheti na Katibu Mkuu wa Chama Chama Tawala cha Msumbiji cha FRELIMO Ndugu Roque Silva Samuel(kulia) tukio hilo ikiwa ni ishara ya kuendeleza ushirikiano na Urafiki kwa Vyama hivyo vyenye Historia kubwa ya Urafiki wa Ukombozi wa Nchini mbali mbali za Afrika,ambapo Hafla hiyo imefanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar leo Tarehe 16/06/2019.
UJUMBE wa Viongozi wa Chama Tawala cha Msumbiji cha FRELIMO wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndugu Roque Silva Samuel wakipewa maelezo katika Eneo la Kihistoria alipouawa kwa kupigwa Risasi na Wapinga Maendeleo Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume April 7, Mwaka 1972.
KATIBU Mkuu wa Chama Tawala cha Msumbiji cha FRELIMO Ndugu Roque Silva Samuel(kulia),akimvisha Kofia Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi ikiwa ni ishara ya Ushirikiano wa kiutendaji baina ya CCM na FRELIMO.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akivishwa Kofia ya FRELIMO na ATIBU Mkuu wa Chama Tawala cha Msumbiji cha FRELIMO Ndugu Roque Silva Samuel, ikiwa ni ishara ya Ushirikiano wa kiutendaji baina ya CCM na FRELIMO.
UJUMBE wa Chama Tawala cha Msumbiji FRELIMO wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndugu Roque Silva Samuel wakiwa na Viongozi wa CCM na Jumuiya zake katika eneo la Kaburi ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume wakiomba Dua.
……………….
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amesema Urafiki wa Vyama vya ASP,TANU na hivi sasa CCM na Chama Cha Tawala cha Msumbiji FRELIMO ni wa Kihistoria uliodumu kwa muda mrefu.
Alisema Urafiki huo umefikia kiwango cha kuwa na uhusiano wa Kindugu na Kidamu baina ya Wananchi wa Nchi hizo mbili,sambamba na kudumisha ushirikiano katika nyanja za Kisiasa na Kidiplomasia.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Ujumbe wa Chama cha FRELIMO ukiongozwa na Katibu Mkuu wake Ndugu Roque Silva Samuel, aliyefika katika Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha mahusiano baina ya Taasisi hizo za Kisiasa.
Dk.Mabodi alisema Chimbuko la Urafiki kati ya Vyama hivyo umetokana na harakati za Vyama vya ASP,TANU na FRELIMO vilivyoongoza harakati za Ukombozi Barani Afrika na baada ya Nchi mbali mbali kupata Uhuru wa kujitawala zenyewe viliendelea kuaminiwa na Wananchi wakavipa ridhaa ya kuongoza Dola.
Alisema kuwa Wananchi wa Msumbiji wanaishi kwa Amani na Utulivu Zanzibar na wapo Wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara wanaoishi Msumbiji kwa Amani masuala yanayotakiwa kuenziwa ili Mahusiano hayo yawe imara zaidi kwa maslahi ya Vizazi vya sasa na Vijavyo.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo alisema Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliongoza Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 na Zanzibar ikawa Huru za kuanza kujitawala yenyewe, ambapo kwa sasa Nchi inaendeleza Mapinduzi ya Kiuchumi kupitia Sera zake imara zilizowekwa na Chama Cha Mapinduzi.
Dk.Mabodi alimwambia Katibu Mkuu huyo kuwa CCM itaendeleza Ushirikiano uliotukuka ulioachwa na Viongozi Wakuu wa Nchi hizo za Msumbiji na Tanzania ambao ni Marehemu Abeid Amani Karume,Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Machel.
Naye Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha Msumbiji Ndugu Roque Silva Samuel,alishukru kwa mapokezi mazuri aliyopata Zanzibar na kueleza kuwa lengo la ziara hiyo fupi ni kuishukru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Msaada waliotoa hivi karibu wakati Msumbiji ilipokumbwa na Maafa.
Alisema Msumbiji ilipata Maafa ya Kimbunga mara mbili na kusababisha Vifo vya Wananchi zaidi ya 600 na kuharibika kwa miundombinu ya Maakaazi,Shule 300,Barabara,Mawasiliano na Nyumba za Umma na binafsi.
“Tunawashukru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa msaada wao Mkubwa waliotoa kwa Msumbiji kwani wameonyesha kwa Vitendo namna wanavyojali
Katibu Mkuu huyo wa FRELIMO alisema Chama hicho kimeendelea kufanya Siasa Huru zinazojali Hali za Watu wote bila ubaguzi wa kabila,rangi na kidini.
Alisema kwa sasa Msumbiji wanajiandaa na Uchaguzi Mkuu wa Dola unaotarajiwa kufanyika Octoba 15,Mwaka 2019,Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa wa huru na haki unakwenda sambamba na Matakwa ya Kidemokrasia.