Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst)
Mhe. George Mkuchika (Mb), alipokuwa akizungumza nao kuhusu
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), akizungumza na
vyombo vya habari jijini Dododma kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa.
********************
Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, inaratibu maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma
Barani Afrika kwa mwaka 2019 ambayo hufanyika mara moja kila baada ya
miaka miwili katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe.
George Mkuchika amesema maadhimisho hayo kwa mwaka huu,
yanatarajiwa kufanyika Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni, 2019.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, malengo ya kuadhimisha siku hii kila
baada ya miaka miwili, ni kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika
kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya Usimamizi wa Utumishi
na Utawala hususan mafanikio na changamoto ili kuzitumia kama chachu ya
kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Mhe Mkuchika amesema, taasisi zitakazoshiriki katika maadhimisho hayo, ni
zile ambazo huduma zake zinalenga moja kwa moja kaulimbiu ya mwaka huu
inayosema “Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa
masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya
TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi,” hivyo kuzitaka
taasisi hizo kuwa mabalozi wazuri katika kuiwakilisha nchi yetu.
Mhe. Mkuchika amezitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni pamoja na
maonyesho ya kazi za ubunifu zilizofanywa na Taasisi kulingana na Kauli
Mbiu, mdahalo kuhusu masuala ya Uwezeshaji wa Vijana, Utawala Bora,
matumizi bora ya TEHAMA, Ubunifu katika utoaji Huduma Jumuishi na namna
bora ya kujenga maadili katika Utumishi wa Umma.
2
Mhe. Mkuchika amesema, katika maadhimisho ya kitaifa, ofisi yake
imewaelekeza Watendaji wa Taasisi za Umma, kukutana na watumishi katika
maeneo yao ya kazi ili kusikiliza maoni na changamoto wanazokutana nazo
katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau
wa nje kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, ili kujenga mahusiano mazuri na jamii,
Taasisi za Umma zinaweza kuadhimisha wiki hiyo kwa kufanya shughuli za
kijamii kama vile za usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali hususan
hospitali, sokoni na katika fukwe za mito na bahari zilizo jirani na maeneo yao
ya kazi.
Sanjari na hayo, Mhe. Mkuchika ameziagiza Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka
za Serikali za Mitaa na Taasisi zote za Umma kuwasilisha taarifa ya namna
walivyoshiriki maadhimisho hayo kwa Makatibu Wakuu wa Wizara ambao
wataunganisha taarifa hizo na kuziwasilisha kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili Serikali iweze kutumia taarifa hizo
kuboresha utendaji kazi.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewapongeza watumishi wote wa umma nchini kwa
kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kuwahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa
manufaa na maendeleo ya Taifa letu.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma husherehekewa na Nchi
Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kila mwaka kuanzia tarehe 16-23 Juni
kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo
ya Nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.