Mkuu wa wilaya ya Kigoma Mh. Samson Anga amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika wilaya ya Kigoma kutokana na hali ya utulivu na usalama uliyopo katika wilaya hiyo.
Amewakaribisha wawekezaji mbalimbali na wafanyabiashara kutoka nchini na nchi jirani za DRC Congo, Zambia, Burundi na maeneo mengine pia kutumia Bandari ya Kigoma kwakuwa mizigo yao mbalimbali watakayosafirisha itafika kwa wakati na kwa gharama nafuu kupitia Bandari hiyo.
Akizungumza na waandishi ofisini kwake Mh. Samson Anga amesema wilaya ya Kigoma kuna utulivu na usalama wa hali ya juu jambo ambalo linaruhusu na kutoa fursa mbalimbali kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao za kibiashara kwa utulivu wilayani humo.
Ameongeza kuwa Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mamlaka ya bandari mkoani Kigoma katika kuboresha miundombinu ya bandari hiyo inatoa wigo na fursa nyingi za uwekezaji kwakuwa usafirishaji wa mizigo mbalimbali ya kibiashara na bidhaa ni rahisi na gharama nafuu zaidi kuliko kutumia usafiri wa barabara.
“Njooni mjenge viwanda, Mfungue mahoteli, Mfanye shughui za utalii, Muwekeze kwenye kilimo na mambo mengine mbalimbali ili kuongeza vipato vyenu kiuchumi na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla” Amesema Mh. Anga.
Amesema, tukishirikiana kwa pamoja tutafanikiwa kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa viwanda ifikapo 2025 kama kauli mbiu ya Rais wetu Dkt. John Pombe Mgufuli inavyosema.