Meneja wa Mamlaka ya Bandari za Ziwa Tanganyika(TPA) Kigoma , Bw. Ajuaye Kheri Msese akizungumza na mmoja wa wananchi wa Kagunga waliolipwa fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara ya kuingia katika bandari hiyo.
Jengo la Soko linalojengwa katika kijiji cha Kagunga kwa ajili ya wafanyabiashara mbalimbali kutoka nchi jirani na mkoa wa Kigoma watakaotumia bandari hiyo.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa soko hilo.
Injinia wa Mamlaka ya Bandari za Ziwa Tanganyika(TPA) Kigoma Nyakato Mwamnana akitoa maagizo kwa mafundi wa kampuni ya Essau Construction inayojenga soko hilo.
……………………………………………………………..
Meneja wa Mamlaka ya Bandari za Ziwa Tanganyika(TPA) Kigoma , Bw. Ajuaye Kheri Msese amesema jumla ya shilingi Bilioni 1.120 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kuingia Bandari ya Kagunga, Fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo na soko linalojengwa bandarini hapo.
Amesema Katika miradi hiyo jumla ya shingili milioni 930 zinanatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kuingia katika bandari ya Kagunga na kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo na milioni 130 zikitumika kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa litakalokuwa na huduma zote.
Bw. Ajuaye Kheri Msese amesema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa mita 700 ni muhimu sana kukamilisha miundombinu ya bandari hiyo kwa sababu upande wa wenzetu kule Burundi wao barabara yao ni nzuri inapitika, lakini kwa upande wetu barabara ya kuingia bandarini lazima tutengeneze ili bandari ya Kagunga ianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Bandari ya Kagunga ilianza kujengwa mwezi Agosti mwaka 2015 na kwa sasa imekamilika kinachoendelea ni ujenzi wa barabara kutoka katika mpaka wa Burundi kwenda bandarini hapo yenye urefu wa mita 700 Pamoja na ujenzi wa soko ambalo litahudumia watu mbalimbali kutoka nchi jirani na watanzania watakaopata huduma ya usafiri kupitia bandari ya Kagunga.
Bandari ya Kagunga ambayo iko kwenye mpaka wa nchi za Burundi na Tanzania mbali ya kuhudumia nchi hiyo kwa usafirishaji wa mizigo mbalimbali pamoja na abiria , Pia itahudumia mizigo kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.