Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya akiwaelezea waandishi wa habari utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Lushamba wakati walipotembelea bandari hiyo jana.(PICHA NA JOHN BUKUKU-FULLSHANGWEBLOG-SENGEREMA)
Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Mwanza (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati walipotembelea bandari ya Lushamba.
Baadhi ya wavuvi wakiwa wameegesha boti zao za uvuvi katika gati la bandari ya Lushamba wilayani Sengerema.
Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Mwanza (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina,akikagua ujenzi wa barabara inayoingia bandarini hapo.
Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya akisaini kitabu cha wageni huku Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Mwanza (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina akiangalia kushoto ni Afisa habari Mwandanizi wa Mamlaka ya Bandari TPA Bw. Leonard Magomba.
Gati la Bandari ya Lushamba linavyoonekana
………………………………………………………………….
NA JOHN BUKUKU -SENGEREMA
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kanyala Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Lazaro Mgonzo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt.John Magufuli kwa kufikiria na kuwajengea bandari ya Lushamba kwa sababu imerahisisha usafiri na biashara za uvuvi pia ni njia mojawapo ya kututangaza na sababu nyingine nyingi katika kurahisisha huduma mbalimbali kisiwani humo.
Mzee Lazaro Mgonzo anasema kuanzia mwaka 1958 hakukuwa na usafiri wa kwenda kisiwani hivyo kujengwa kwa bandari hiyo na kuanza kwa usafiri kutatatua changamoto mbalimbali kisiwani humo.
“Tunashukuru serikali kwa kutukumbuka kwa ujenzi wa bandari ambayo itarahisisha usafiri wa kuja na kutoka kisiwani ambao kwa miaka mingi umekuwa na changamoto nyingi,” alisema.
Naye Mtendaji wa kijiji hicho, Benjamin Nhnugwizi, amewataka wananchi wakazi wapatao 8,798 wa kijiji hicho kutunza miundombinu ya bandari hiyo ambayo inategemewa na vitongoji vinne vya Mwibale, Msikitini, Kisarazi na Gembale kwa sababu pia itatoa ajira kwa vijana wa maeneo hayo kuzunguka kijiji.
Bandari hiyo imejengwa baada ya miaka 61 ya adha ya usafiri wa majini katika kisiwa hicho na vingene vya karibu.
Awali, Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya alisema Ujenzi wa Bandari ya Lushamba umekamilika kwa asilimia 90 na umegharimu Sh. bilioni 1.265 ambazo ni fedha za ndani, itaanza kutumika Julai mwaka huu baada ya usafiri huo kuwa wa kusuasua tangu mwaka 1958.
Utekelezaji unaendelea ambapo sehemu iliyobaki ni kumalizia ujenzi wa jengo la abiria, jengo la kuhifadhia mizigo, uzio, vyoo mnara wa tanki la maji na chumba cha mashine ya umeme.
“Ni bandari ndogo, nzuri na ya kisasa kwa sababu imejengwa kwa viwango vya kimataifa, tunategemea wananchi wengi zaidi kuitumia bandari hii,” alisema.
Kwa upande wake Injinia wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Mwanza (TPA), Kanda ya Ziwa Victoria, Abraham Msina, alisema gati hilo lina urefu wa mita 60 ambapo wakati wa ujenzi wake nyumba nne za wananchi zililipwa fidia ili kupisha mradi huo.
“Mradi huu ni wa mwaka mmoja ambapo tunategemea mkandarasi kuukabidhi Julai 9, mwaka huu na hatutegemei kuongeza muda,” alisema.