Baadhi ya wanafunzi wa shule ya awali na msingi Tarangire ya Mjini Babati Mkoani Manyara, wakiwa kwenye basi la shule yao tayari kurudi majumbani mwao kwa ajili ya mapumziko jana.
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Fachakademien cha nchini Ujerumani wakiwa kwenye shule ya Tarangire Pre and Primary English Medium ya mjini Babati Mkoani Manyara, ambapo wanafundisha kwa kujitolea.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya awali na msingi Tarangire ya mjini Babati Mkoani Manyara wakiwa kwenye mazingira ya shule hiyo.
*****************************************
KATIKA kushiriki mafunzo kwa vitendo wanafunzi wa chuo kikuu cha Fachakademien wa nchini Ujerumani wamejitolea kuwafundisha wanafunzi wa shule ya Tarangire Pre & Primary English Medium ya Mjini Babati Mkoani Manyara, kwenye kufanikisha ushirikiano na mahusiano mema.
Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya Tarangire, Eva Mrutu akizungumza jana alisema wamefarijika kupata ugeni huo kutoka nchini Ujerumani ambao kwa namna moja au nyingine wamewaongezea ujuzi wanafunzi wao.
Mrutu alisema wageni hao kutoka Ujerumani wamewafundisha wanafunzi wao mambo mapya ambayo walikuwa hawajafundishwa.
“Wanafunzi wetu wamefurahi kupata mambo mapya ikiwemo michezo na nyimbo mbalimbali ambazo hawakuwahi kuziimba ila zimewaongezea morali ya kusoma zaidi” alisema Mrutu.
Mmoja kati ya wanafunzi hao wa chuo kikuu cha Fachakademien Rebecca Steve alisema hii ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania na amefurahishwa na ukarimu ulioonyeshwa kwao.
“Tutarudi, tena hapa nchini Tanzania kwani watu wake ni wakarimu, wema na wenye upendo kwa wageni kwa hakika tunefurahi mno kufika hapa shule ya Tarangire,” alisema Rebecca.
Mwanafunzi wa darasa la nne kwenye shule hiyo ya Tarangire, Jackline Peter alisema walimu hao kutoka nchini Ujerumani walimfundisha kuchora na kuchanganya rangi.
Mwanafunzi wa darasa la tatu Philipo Tabari alisema alifurahia nyimbo mpya walizofundishwa ikiwemo wimbo wa tembo ni mnyama mzuri.
Mwalimu wa kitengo cha masoko, Judith Misana alisema shule yao ipo kwenye miteremko ya mlima Kwaraa mjini Babati barabara kuubya Mamire karibu na chuo cha Veta Manyara.
“Wazazi na walezi tinawakaribisha wote waleteni watoto wapate elimu nzuri hapa kwetu Tarangire kupitia kauli mbiu ya shule yetu ya juhudi katika kutafuta elimu na Mungu,” alisema Misana.
Alisema shule hiyo ina wana walimu wazuri wenye kufundisha masomo bora, mabasi ya kusafirisha wanafunzi kila siku, vyakula vizuri wanavyolima wenyewe na sehemu nzuri za kulala.