Home Mchanganyiko RC CHRISTOPHER OLE SENDEKA AKABIDHI TUZO UHIFADHI WA MAZINGIRA MIKOA YA IRINGA...

RC CHRISTOPHER OLE SENDEKA AKABIDHI TUZO UHIFADHI WA MAZINGIRA MIKOA YA IRINGA , NJOMBE NA MBEYA AAGIZA WATENDAJI WAZEMBE KUWAJIBISHWA

0

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiindi wa tuzo za uhifadhi mazingira na waratibu na viongozi mbali mbali

Mwakilishi wa kituo cha Radio Ebony FM Maregesi Gilsoni akikabidhiwa cheti na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka

********************************************

Na Francis Godwin, Njombe 
MKUU  wa  mkoa wa  Njombe Chistopher Ole Sendeka  ameagiza   wakuu  wa  kuwachukulia  hatua  kali watendaji  wa kata  ambazo  zimeshindwa  kurejesha  fomu  zilizotolewa  kwa  watendaji wa  kata zote za mikoa ya Iringa , Njombe na Mbeya kwa ajili ya ushiriki wa  tuzo ya hifadhi  za  Taifa (TANAPA) hifadhi ya Ruaha  tuzo ya kuhifadhi mazingira mwaka  2019.

Akizungumza  jana katika  kijiji  cha  Magoye wilayani Makete  mkoani Njombe wakati wa  kilele  cha shindano  la  tuzo  za Tanapa   ya  kuhifadhi  mazingira  kwa  mwaka 2019 , mkuu   huyo  wa  mkoa  alisema  lengo la  kuanzisha   tuzo  hizo ni  utekelezaji  wa agizo la  serikali ya  awamu ya tano  chini ya rais Dkt John Magufuli   hivyo  kitendo cha  baadhi ya  watendaji  kukwamisha  zoezi   hilo  ni  kosa na  lazima  hatua  kali zichukuliwe  dhidi  yao .

Alisema  kuwa  pamoja na  taarifa  za  waandaaji  wa  tuzo  hizo  kuonyesha  idadi ya  washiriki  wa  shindano la  tuzo  hizo  imezidii  kuongezeka  ila  kumekuwepo na  malalamiko  kutoka kwa   wananchi  kushindwa  kufikishiwa  fomu  za    shindano  hilo  kutoka  kwa  watendaji wa kata  ambao  walikabidhiwa  fomu  ili  kuzigawa  kwa  wananchi  wote  jambo ambalo ni ukiukaji wa agizo la  serikali la  utunzaji wa mazingira  nchini .

“ Kwa  kuwa  fomu  hizi  zimetolewa  kwa  watendaji wa kata  zote  za  wilaya za  Mbarali , Makete ,  wanging’ombe , Kilolo  na Mufindi  lengo  lilikuwa ni  kuona  wananchi  wa kata  zote  wanashirikishwa  kikamilifu katika  shindano  hilo  ila  yapo malalamiko  kuwa  wananchi  baadhi  wameshindwa  kufikishiwa  fomu  hizo na baadhi ya  watendaji  sasa naagiza  wakuu wa wilaya kuwatafuta  watendaji hao  ambao  wameshindwa  kufikisha  fomu hizo  kwa wananchi  na  kuwachukulia  hatua ili  iwe  fundisho kwa  wakati  mwingine  kwa  kila mmoja   kutekeleza  agizo la uhifadhi wa mazingira  na mimi katika mkoa wangu watendaji hawa nitataka  wachukuliwe  hatua “  alisema ole Sendeka.

Alisema  kuwa   suala la  uhifadhi  wa mazingira  si  suala la  mchezo wala  la  utani kwani  kila mtanzania  ni mhifadhi  na   jitihada  zinazoonyeshwa na  serikali  chini ya rais Dkt Magufuli ambae  yeye na makamu  wake wa rais  ni  wahifadhi  namba  moja  hivyo  lazima   kila  mmoja  kuunga mkono  jjitihada  hizo  kwa  kushiriki  utunzaji wa mazingira .

“  Mheshimiwa  rais  wetu  Dkt  Magufuli kama  mhifadhi  mazingira  namba  moja  kazi  hii amemkabidhi  makamu   wa  rais  mama  Samia  Suluhu  Hassan ambae  kila  mmoja  amekuwa  akishuhudia kazi  kubwa  ambayo amekuwa akiifanya  ikiwa ni pamoja na kutuita  wakuu wa  mkoa wote wa mikoa ya nyanda za  juu  kusini  pamoja na  wakuu wa wilaya  ili kuokoa  Ikolojia ya mtu  Ruaha  mkuu   hivyo  hatuna  mchezo na kazi  hii “  alisema  mkuu  huyo wa  mkoa.

Alisema  kuwa  kilimo  endelevu  ,uvuvi  endelevu na  uvunaji  miti  endelevu  vyote  vinawezekana  iwapo  kila  mmoja atachukua  jukumu la  kuwa mhifadhi wa mazingira  yanayomzunguka  katika maeneo yake  na  suala la  ushirikishwa wa wananchi  kwenye  tuzo  hizo za Tanapa ni jukumu la  viongozi  wote  wa  vijiji na kata .

Aidha  aliwapongeza  wakuu  wa  mikoa ya  Iringa , Mbeya   na  wakuu  wote  wa  wilaya   hizo na  wakurugenzi  ambao kwa  pamoja  wamefanikisha  maeneo yao  kushiriki  tuzo  hizo nakushindwa  kwa miaka  yote  mitatu  mfululizo  toka  kuanzishwe kwa shindano la  tuzo  hizo za uhifadhi wa mazingira na kutaka uhamasishaji  kuendelea  zaidi  ili idadi ya  washiriki  idizi  kuwa  juu .

Meneja wa Miradi ya Ujirani Mwema wa  TANAPA , Ahmed Mbugi  alisema kuwa   mpango  wa tuzo  hizo  ulianza   kutekelezwa  mwaka  2016 katika  wilaya tano  za  mikoa ya  Iringa , Mbeya na  Njombe   na  kuwa na washiriki 56 ,mwaka  2017  idadi ya  washiriki  iliongezeka na kufikia  jumla ya washiriki 171 ,mwaka  2018  washiriki  245 na  mwaka  huu  2019  idadi imeongezeka  zaidi na kufikia  washiriki  680.

Alisema  washirikiki  waliojitokeza ni  watumiaji maji ,shule , serikali  za  vijiji ,watu  binafsi  pamoja na taasisi  binafsi  zinazofanya kazi ya  uhifadhi wa mazingira, utoaji elimu na upandaji  miti  ya  uhifadhi wa misitu ya  asili   ,uhifadhi wa  ardhi  na uhifadhi wa mazingira na wanyamapori .

Hata   hivyo  alisema  pamoja na TANAPA  kuwezesha  shindano  hilo  pia wadau  mbali mbali  wamekuwa  wakijitokeza  kuwezesha  ambao ni  halmashauri   ya  Kilolo, Mufindi, Makete ,Mbarali , wanging’ombe na  washirika wengine kama  Regrow Tanzania , shirika la mazingira  Duniani (WWF) malihai Club of Tanzania  Nyanda za  juu  kusini bonde la maji   Rufuji  .

Pia  vyombo  vya habari  ambavyo  vimeweza  kutoa  mchango  mkubwa katika kuhamasisha  jamii  kutambua  na  kushiriki  tuzo  za  uhifadhi wa mazingira .

Akizungumza  kwa niaba ya  mkuu  wa  mkoa wa  Iringa  katika  kilele  cha  utoaji  tuzo  hizo mkuu wa  wilaya ya  Kilolo  Asia  Abdalah  alisema kuwa mkoa  wa  Iringa  umejipanga  kuendelea  kuhifadhi mazingira  na  tayari  umekuwa  ukitekeleza  maagizo mbali mbali ya  serikali katika  utunzaji  na  uendelezaji wa  mazingira  .

Aidha  alisema  suala la  elimu ya  utunzaji wa  misitu  imeendelea  kutolewa na  kutoa  elimu ya  wananchi  kuepuka  uchomaji moto  misitu  pia  kuhamasisha  wananchi  kuendelea  kutumia  mifuko  mbadala  badala ya  kutumia  mifuko ya  rambo  isiyo  rafiki na mazingira .

Mwandamizi mratibu  wa  tuzo   ya  TANAPA hifadhi ya Ruaha  katika  uhifadhi wa mazingira  mwaka 2019 Yassin  Sharif ambae  ni aliwataja  washindi wa kwanza  kwa  kila  wilaya  ambao walikabidhiwa   cheti pamoja na  hundi ya  shilingi  milioni 2  kuwa ni  Lenatusi  Sublime  kutoka  kijiji cha Wotalisoli  wilaya ya  Kilolo  , kijiji  cha  Ugute  wilaya ya  Mufindi , Jumuiya  ya  watumiaji maji  Mbumtilu  wilayani Wanging’ombe , shule ya  sekondari  Mengele  wilaya ya  Mbarali  na kwa  wilaya ya makete  ni Shule ya  sekondari Mlondwe .

Wakati  washindi wa  pili ambao walipata   hundi ya  shilingi  milioni 1.5  na  cheti   kutoka wilaya ya  Kilolo  ni  kijiji cha Ikula ,  wilaya ya  Mufindi  Kikundi cha Igomaa, wilaya ya  wanging’ombe   Atukuzwe  Erasto , wilaya ya  Mbarali  Ambokile Twikasyege  na  wilaya ya Makete  ni  Jacob Sanga .

Washindi wa tatu katika  kila wilaya  ambao  walizawadiwa  cheti na hundi ya  shilingi  milioni  1  kila mmoja   kwa  wilaya ya  Kilolo ni  kamati ya maliasili na mazingira  kijiji cha Msosa ,  wilaya ya  Mufindi  shule ya msingi  langamoto ,  wilaya ya  wanging’ombe  Kijiji cha Makoga , wilaya ya Mbarali  Jumuiya ya  watumia maji  mto  Mbarali na  wilaya ya akete  ni  kijiji cha Ikuwo .