Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiindi wa tuzo za uhifadhi mazingira na waratibu na viongozi mbali mbali
Mwakilishi wa kituo cha Radio Ebony FM Maregesi Gilsoni akikabidhiwa cheti na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka
********************************************
Akizungumza jana katika kijiji cha Magoye wilayani Makete mkoani Njombe wakati wa kilele cha shindano la tuzo za Tanapa ya kuhifadhi mazingira kwa mwaka 2019 , mkuu huyo wa mkoa alisema lengo la kuanzisha tuzo hizo ni utekelezaji wa agizo la serikali ya awamu ya tano chini ya rais Dkt John Magufuli hivyo kitendo cha baadhi ya watendaji kukwamisha zoezi hilo ni kosa na lazima hatua kali zichukuliwe dhidi yao .
Alisema kuwa pamoja na taarifa za waandaaji wa tuzo hizo kuonyesha idadi ya washiriki wa shindano la tuzo hizo imezidii kuongezeka ila kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kushindwa kufikishiwa fomu za shindano hilo kutoka kwa watendaji wa kata ambao walikabidhiwa fomu ili kuzigawa kwa wananchi wote jambo ambalo ni ukiukaji wa agizo la serikali la utunzaji wa mazingira nchini .
“ Kwa kuwa fomu hizi zimetolewa kwa watendaji wa kata zote za wilaya za Mbarali , Makete , wanging’ombe , Kilolo na Mufindi lengo lilikuwa ni kuona wananchi wa kata zote wanashirikishwa kikamilifu katika shindano hilo ila yapo malalamiko kuwa wananchi baadhi wameshindwa kufikishiwa fomu hizo na baadhi ya watendaji sasa naagiza wakuu wa wilaya kuwatafuta watendaji hao ambao wameshindwa kufikisha fomu hizo kwa wananchi na kuwachukulia hatua ili iwe fundisho kwa wakati mwingine kwa kila mmoja kutekeleza agizo la uhifadhi wa mazingira na mimi katika mkoa wangu watendaji hawa nitataka wachukuliwe hatua “ alisema ole Sendeka.
Alisema kuwa suala la uhifadhi wa mazingira si suala la mchezo wala la utani kwani kila mtanzania ni mhifadhi na jitihada zinazoonyeshwa na serikali chini ya rais Dkt Magufuli ambae yeye na makamu wake wa rais ni wahifadhi namba moja hivyo lazima kila mmoja kuunga mkono jjitihada hizo kwa kushiriki utunzaji wa mazingira .
“ Mheshimiwa rais wetu Dkt Magufuli kama mhifadhi mazingira namba moja kazi hii amemkabidhi makamu wa rais mama Samia Suluhu Hassan ambae kila mmoja amekuwa akishuhudia kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya ikiwa ni pamoja na kutuita wakuu wa mkoa wote wa mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na wakuu wa wilaya ili kuokoa Ikolojia ya mtu Ruaha mkuu hivyo hatuna mchezo na kazi hii “ alisema mkuu huyo wa mkoa.
Alisema kuwa kilimo endelevu ,uvuvi endelevu na uvunaji miti endelevu vyote vinawezekana iwapo kila mmoja atachukua jukumu la kuwa mhifadhi wa mazingira yanayomzunguka katika maeneo yake na suala la ushirikishwa wa wananchi kwenye tuzo hizo za Tanapa ni jukumu la viongozi wote wa vijiji na kata .
Aidha aliwapongeza wakuu wa mikoa ya Iringa , Mbeya na wakuu wote wa wilaya hizo na wakurugenzi ambao kwa pamoja wamefanikisha maeneo yao kushiriki tuzo hizo nakushindwa kwa miaka yote mitatu mfululizo toka kuanzishwe kwa shindano la tuzo hizo za uhifadhi wa mazingira na kutaka uhamasishaji kuendelea zaidi ili idadi ya washiriki idizi kuwa juu .
Meneja wa Miradi ya Ujirani Mwema wa TANAPA , Ahmed Mbugi alisema kuwa mpango wa tuzo hizo ulianza kutekelezwa mwaka 2016 katika wilaya tano za mikoa ya Iringa , Mbeya na Njombe na kuwa na washiriki 56 ,mwaka 2017 idadi ya washiriki iliongezeka na kufikia jumla ya washiriki 171 ,mwaka 2018 washiriki 245 na mwaka huu 2019 idadi imeongezeka zaidi na kufikia washiriki 680.
Alisema washirikiki waliojitokeza ni watumiaji maji ,shule , serikali za vijiji ,watu binafsi pamoja na taasisi binafsi zinazofanya kazi ya uhifadhi wa mazingira, utoaji elimu na upandaji miti ya uhifadhi wa misitu ya asili ,uhifadhi wa ardhi na uhifadhi wa mazingira na wanyamapori .
Hata hivyo alisema pamoja na TANAPA kuwezesha shindano hilo pia wadau mbali mbali wamekuwa wakijitokeza kuwezesha ambao ni halmashauri ya Kilolo, Mufindi, Makete ,Mbarali , wanging’ombe na washirika wengine kama Regrow Tanzania , shirika la mazingira Duniani (WWF) malihai Club of Tanzania Nyanda za juu kusini bonde la maji Rufuji .
Pia vyombo vya habari ambavyo vimeweza kutoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kutambua na kushiriki tuzo za uhifadhi wa mazingira .
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa katika kilele cha utoaji tuzo hizo mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah alisema kuwa mkoa wa Iringa umejipanga kuendelea kuhifadhi mazingira na tayari umekuwa ukitekeleza maagizo mbali mbali ya serikali katika utunzaji na uendelezaji wa mazingira .
Aidha alisema suala la elimu ya utunzaji wa misitu imeendelea kutolewa na kutoa elimu ya wananchi kuepuka uchomaji moto misitu pia kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia mifuko mbadala badala ya kutumia mifuko ya rambo isiyo rafiki na mazingira .
Mwandamizi mratibu wa tuzo ya TANAPA hifadhi ya Ruaha katika uhifadhi wa mazingira mwaka 2019 Yassin Sharif ambae ni aliwataja washindi wa kwanza kwa kila wilaya ambao walikabidhiwa cheti pamoja na hundi ya shilingi milioni 2 kuwa ni Lenatusi Sublime kutoka kijiji cha Wotalisoli wilaya ya Kilolo , kijiji cha Ugute wilaya ya Mufindi , Jumuiya ya watumiaji maji Mbumtilu wilayani Wanging’ombe , shule ya sekondari Mengele wilaya ya Mbarali na kwa wilaya ya makete ni Shule ya sekondari Mlondwe .
Wakati washindi wa pili ambao walipata hundi ya shilingi milioni 1.5 na cheti kutoka wilaya ya Kilolo ni kijiji cha Ikula , wilaya ya Mufindi Kikundi cha Igomaa, wilaya ya wanging’ombe Atukuzwe Erasto , wilaya ya Mbarali Ambokile Twikasyege na wilaya ya Makete ni Jacob Sanga .
Washindi wa tatu katika kila wilaya ambao walizawadiwa cheti na hundi ya shilingi milioni 1 kila mmoja kwa wilaya ya Kilolo ni kamati ya maliasili na mazingira kijiji cha Msosa , wilaya ya Mufindi shule ya msingi langamoto , wilaya ya wanging’ombe Kijiji cha Makoga , wilaya ya Mbarali Jumuiya ya watumia maji mto Mbarali na wilaya ya akete ni kijiji cha Ikuwo .