Na Happy Lazaro, Arusha

Wafanyabiashara nchini wameiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa ukusanyaji wa service levy unaotozwa na Serikali za Mitaa, wakieleza kuwa utaratibu huo umekuwa ukiwaongezea mzigo wafanyabiashara na kuathiri shughuli zao za biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (Ombudsman) ,Mjumbe wa bodi ya wadhamini jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania , Geoffrey Kirenga amesema kuwa , jukwaa hilo limekuwa muhimu kwa kuwa limewapa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho la pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi.

Kirenga amesema kuwa kupitia majadiliano hayo, wanaamini kuna uwezekano wa kupata afueni kwa wafanyabiashara wengi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na kodi na tozo.

Ameongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya maeneo, kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wafanyabiashara wanaona kuna maboresho katika utendaji wake na kwamba changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ipo zaidi kwenye baadhi ya tozo zinazotozwa na Serikali za Mitaa, hususan service levy.

Amefafanua kuwa tatizo kubwa ni namna service levy inavyokadiriwa, ambapo kwa mtazamo wao, tozo hiyo inapokuwa inahesabiwa kwa kuangalia jumla ya mauzo badala ya kuzingatia hali halisi ya biashara, inaweza kumuumiza mfanyabiashara ambaye huenda hana faida kubwa.

“Service levy imekuwa ni moja ambayo inawafanya wafanyabiashara kuwa maskini, kwa sababu wanapopiga ile percentage yao, wanapigia kwenye mfumo ambao ni wa jumla. Siyo faida, siyo hasara, siyo mkopo; wanachukulia flat rate,” amesema Kirenga .

Amesema mfumo huo unaweza kumuweka mfanyabiashara katika mazingira magumu kwa sababu biashara inaweza kuwa na mauzo makubwa lakini faida yake ikawa ndogo kutokana na gharama mbalimbali za uendeshaji.

Aidha, amesema hatua za sasa za kuanza kutumia mfumo wa makadirio badala ya utaratibu uliokuwa ukitumika awali zimeongeza hofu miongoni mwa wafanyabiashara, hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha mabadiliko yoyote katika mfumo wa kodi yanafanyika kwa kuzingatia uhalisia wa biashara na uwezo wa mfanyabiashara.

Amesisitiza kuwa iwapo Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya kodi na tozo kwa kuzingatia uwezo halisi wa wafanyabiashara, hatua hiyo inaweza kusaidia kukuza biashara, kuongeza uaminifu kati ya Serikali na sekta binafsi na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali kwa njia endelevu.