************************************************
NA MWAMVUA MWINYI,KISARAWE
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Pwani Kamishina Msaidizi (ACP) ,Wankyo Nyigesa, ametoa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele kilo 100,sukari kilo 50 ,juice,mafuta ya kula na fedha katika kituo cha kulelea watoto yatima huko Sanze ,kata ya Kazimzumbwi,Kisarawe ikiwa ni kuelekea sikukuu ya Eid el fitri.
Akiwa kituoni hapo pia aliungana na watoto wenye mahitaji maalum katika kwenye iftari ya pamoja na jeshi hilo .
Akizungumza na waandishi wa habari,Wankyo aliwaambia kwamba ,ni utamaduni wa kawaida kwa jeshi la polisi mkoa kujumuika na watoto yatima,wadau na makundi maalum katika jamii kwenye kipindi hiki cha mfungo.
Alieleza, tayari Jeshi la Polisi mkoani hapo limeftarisha katika wilaya ya Kibaha ,wadau mbalimbali na katika kuendeleza utamaduni waliojiwekea likaona ipo haja ya kuftari na watoto wenye uhitaji.
“Katika kuhakikisha watoto hao wanasherekea sikukuu ya Eid el fitri kwa furaha, Jeshi hili Mkoa wa Pwani limetoa vitu mbalimbali kama mchele, mbuzi, mafuta ya kula, sabuni, sukari, chumvi, juice na fedha”alifafanua Wankyo.
Nae msimamizi wa kituo hicho, Florida Frank, alielezea,Jeshi hilo limeonyesha mfano kwa taasisi zingine ndani ya serikali kwa kitendo cha kuwakimbilia na kuftari pamoja na kutoa mkono wa Eid kwa watoto hao jambo ambalo litawafanya kusherekea Eid kwa furaha.
“Kituo hiki ,kina watoto 26 kati yao wa kiume ni 15 na wa kike 11 wakiwa na walezi sita , na kilianzishwa toka mwaka 2007″alieleza Florida.
Alisema wapo watoto wenye umri kati ya miak 04 hadi 22 wanaosoma shule za chekechea 04, msingi 10, sekondari 08, cheti 01, na wasiosoma 03 bado wanaandaliwa utaratibu wa elimu na kituo kinajiendesha kwa kufanya ujasiliamali wa kutengeneza batiki na taulo za wanawake.