Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amefuturisha maelfu ya watu wenye ulemavu na wasiojiweza kama sehemu ya sadaka yake ya Ramadhani na kumuenzi aliekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Marehemu Dkt. Reginald Mengi aliefariki hivi karibuni.
Katika futari hiyo RC Makonda amewapa hadhi ya juu watu wenye walemavu baada ya kuwaalika watu mashuhuri nchini wakiwemo wasanii wa kubwa, waigizaji,wachekeshaji,madaktari, makamanda, vyombo vya ulinzi na usalama na kuwapa jukumu moja la kuhakikisha wanahudumia watu wenye ulemavu vyakula, vinywaji na kuwasikiliza shida zao jambo ambalo walemavu wamelizungumzia kama heshima ya kipekee wamepatiwa.
RC Makonda ameeleza kuwa futari hiyo ni sehemu ya safari ya kutimia ahadi yake ya kumuenzi Marehemu Mengi kwa upendo,ukarimu, unyenyekevu na moyo wa kujitoa kusaidi makundi ya wasiojiweza huku akieleza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.
Aidha RC Makonda amewahimiza wananchi kuwa na moyo wa upendo na kusaidia makundi ya wasiojiweza kwakuwa anaamini kwa kufanya hivyo watachuma baraka.
Pamoja na hayo RC Makonda amewaomba wananchi kuliombea Taifa na Viongozi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli ambae amekuwa mtetezi wa wanyonge na mpiganaji wa maendeleo kwa maslahi ya wote.