Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa kikao cha dharura na Wakurugenzi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Wizara ya Kilimo kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo katika mji wa serikali Ihumwa Jijini dodoma leo tarehe 31 Mei 2019. Wengine pichani ni Naibu Waziri Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe pamoja na na Prof Siza Tumbo, Naibu katibu Mkuu.
****************************************
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 31 Mei 2019 ameitisha kikao cha dharura na Wakurugenzi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Wizara ya Kilimo lengo ni kuanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuiuzia nchi ya Zimbabwe mahindi na mazao mengine kiasi cha Tani Laki Nane (800,000).
Itakumbukwa mapema wiki hii, Rais John Pombe Magufuli alipoitembelea Zimbabwe kwa mwaliko wa Mwenyeji wake Rais Emmerson Mnangagwa. Rais Mnangagwa alimweleza Rais Magufuli kuwa Zimbabwe inakabiliwa na upungufu wa chakula na kuiomba Tanzania iiuzie sehemu ya chakula chake cha ziada ombi ambalo Rais Magufuli alilikubali.
Waziri Hasunga amesema ujumbe kutoka Serikali ya Zimbabwe utawasili nchini kuanzia Siku ya Jumanne ya Tarehe 3 Juni na unatajiwa kuwa nchini mpaka tarehe 7 ya Mwezi Juni, 2019.
Waziri Hasunga ameongeza kuwa ujumbe huo kutoka Zimbabwe unakuja kwa ajili ya kuangalia na kujiridhisha kuhusu mambo ya msingi kama ubora wa chakula na mambo mengine ya awali.
Waziri wa Kilimo amesema kimsingi Serikali zote mbili zimekubaliana kuwasaidia Wananchi kwa njia ya biashara na kuongeza kuwa huu ni mwanzo kwa kufanya biashara endelevu baina ya nchi hizi mbili na kuongeza kwa biashara hiyo, itakuwa endelevu mwaka hadi mwaka.
Mhe. Hasunga amesema Zimbabwe imefikiria pia kuanza kununua mazao mengine kama korosho kwa kuwa imeona fursa ya kupata mazao yenye ubora na kwa bei nzuri ipo Tanzania kwamba baadae mazao mengine ya mbegu za mafuta, jamii ya mikunde, mboga na matunda yataanza kununuliwa na Taifa hilo la Kusini mwa Afrika.