Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameipongeza Benki ya CRDB kwakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za ujenzi wa taifa kupitia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa mradi wa ufuaji umeme wa Stiglers gogle na mingine mingi.
Spika Ndugai aliyasema hayo wakati wa futari maalum iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake jijini Dodoma.
“Tuna imani kubwa na Benki ya CRDB. Siku zote nimekuwa nikisisita kuwa Benki hii ndio kioo halisi cha mabenki yetu nchini. Mafanikio ya Benki ya CRDB yana akisi hali halisi ya uchumi wa taifa na mtanzania mmoja mmoja. Hivyo basi, sisi kama Bunge tutaendelea kuwapa kila ushirikiano unaohitajika. Watanzania wanajisikia fahari kuona Benki yao ya kizalendo kiendelea kuimarika.”
Kwa niaba ya wageni waalikwa ambao walihusisha Mawaziri, Wabunge na wateja wa benki ya CRDB, Mheshimiwa Ndugai aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuundaa futari hiyo maalum jijini Dodoma. “Tunawashukuru benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa kuandaa futari kwa ajili ya wateja wadau wake hapa Dodoma. Sisi watu wa Dodoma tunaona ufahari kwa kitendo hiki kwani kinaonesha kuwa mnatujali, Ahsanteni sana” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela aliwashukuru wageni waalikwa kwa kuhudhuria futari hiyo na kuwaahidi kuendelea kuboresha huduma za benki ya CRDB ili kufikia matarajio yao. “Kipekee kabisa niwashukuru wageni wote mliofika hapa leo.
Benki ya CRDB tumejiwekea utaratibu kila mwaka wa kushiriki katika futari ili kuungana na ndugu zetu wa kiislamu katika kuomba dua pamoja na kuomba yaliyo mema. Nichukue nafasi kuwaahidi kuwa tutaendelea kuwa wabunifu huku tukiongeza utumiaji wa mifumo ya kidijitali ili tuweze kuwapa huduma zitakazokidhi matarajio yenu. Sisi benki ya CRDB tunandelea kuwaahidi huduma bora zaidi na ahadi yetu kwenu ni kuwa TUPO TAYARI KUWAHUDUMIA”.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela baada ya hafla ya Iftar iliyoandalia na Benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wa Jijini Dodoma, iliyofanyika katika Hoteli ya Morena, jana Mei 29, 2019. Kulia ni Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Ally Laay.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakimsikiliza, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya hafla ya Iftar iliyoandalia na Benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wa Jijini Dodoma, iliyofanyika katika Hoteli ya Morena, jana Mei 29, 2019.