Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Dk Rashid Tamatama,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma mara baada ya kufanya mazungumzo na wafadhili wa Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kutoka Karea Kusini
Mkurugenzi wa Sekta ya Uvuvi, Magesa Bulayi,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma mara baada ya kufanya mazungumzo na wafadhili wa Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kutoka Karea Kusini
Mazungumzo yakiendelea kufanyika kati ya Picha ya pamoja ya Wizara za Fedha,Mifugo na Uvuvi pamoja na wafadhili wa Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kutoka Nchini Korea Kusini
Picha ya pamoja ya ujumbe toka Korea na Wizara za Fedha,Mifugo na Uvuvi leo katika UKumbi wa Hazina leo.
Picha na Alex Sonna-Fullshangweblog
……………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Dk Rashid Tamatama,amesema kuwa sekta ya Uvuvi nchini ipo katika hatua ya mchakato wa kujenga Bandari za Uvuvi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa samaki, uchakataji na uuzaji kwenye masoko ya uhakika la mazao yake ndani na nje ya nchi.
Dk.Tamatama ameyasema hayo leo jijini Dodoma mara baada ya kufanya mazungumzo na wafadhili wa Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kutoka Nchini Korea Kusini.
Amesema kuwa taarifa hiyo ikiwasilishwa itakuwa imebainisha ni wapi bandari hizo zitajengwa katika mwambao wa Tanga hadi Mtwara pamoja na Zanzibar pamoja na gharama halisi za ujenzi wake.
Aidha Dk.Tamatama amesema kuwa wizara hiyo imeelekezwa kupanua uwigo wa uvuvi kwa kujenga bandari za uvuvi na mkakati huo upo ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Serikali wa miaka mitano 2016/17-2020/21 na katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Hata hivyo ameongeza kuwa ili kutekeleza mradi huo sekta hiyo imewaalika wafadhili kufika nchini na wamefika na kufanya mazungumzo na wizara ya Fedha na Mipango baadaye watafanya na wizara husika na watatembelea maeneo ya Pwani na hata Zanzibar.
Ametaja kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na maeneo makubwa ya maji, yakiwemo maji baridi ya maziwa matatu makubwa ambapo inamiliki asilimia 51 ya Ziwa Victoria, asilimia 41 Ziwa Tanganyika na asilimia 18 ya Ziwa Nyasa.
Dk Tamatama amesema kuwa pamoja na kuwa na raslimali kubwa ya maji, sekta ya uvuvi inatoa mchango mdogo katika pato la taifa, hivyo mkakati wa ujenzi wa bandari za uvuvi utachangia katika kuongeza pato la taifa lakini hasa kuwa na uhakika wa soko la uhakika la mazao ya bidhaa hiyo.
Amesema kuwa mwaka 2017 serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, na taarifa itakamilika Juni mwaka huu, kwa sasa wizara inatafuta fedha ndiyo maana imewaalika wafadhili kutoka Korea Kusini mara baada ya kupewa idhini na wizara ya fedha kufanyika kwa mradi huo kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sekta ya Uvuvi, Magesa Bulayi amesema kuwa wizara hiyo kupitia sekta ya uvuvi, imejipanga kusonga mbele na kuhakikisha nchi inapata faida kutokana na kuwepo kwa samaki katika maziwa na bahari nchini.
Bw.Bulayi amesema kuwa ili kufanikisha azma hiyo, wizara inaandaa miundombinu ya bandari ambazo zitakuwa chanzo cha uhakika wa upatikanaji wa mazao ya samaki, masoko, kupunguza uvuvi haramu na kuongeza thamani ya mazao ya samaki katika mnyororo mzima wa uchakataji mazao hayo.
“Pia itasaidia kutunza samaki, kupata takwimu sahihi na za uhakika kuhusu idadi na kiwango cha samaki wanaovuliwa na kuwa na soko la uhakika la kuuza katika bandari hiyo,” amesema Bulayi.
Ujumbe wa Watalaamu tisa wa masuala ya uvuvi kutoka Korea Kusini uliongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Mwandamizi kutoka Wizara ya Bahari na Uvuvi, Kim, Sung Ho amesisitiza kuwa mkakati wao wa kusaidia Tanzania katika kuongeza thamani mazao ya samaki kutokana na kujengwa kwa bandari hizo.