NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo amekemea baadhi ya madiwani kuacha kuingiza siasa kwenye shughuli za wataalamu ,katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa hospital za wilaya unaoendelea kujengwa kwenye halmashauri tatu za mkoa huo .
Aidha amezitaka, halmashauri zinazojengwa hospital hizo ikiwemo Kibaha Mji,Kibiti na halmashauri ya wilaya ya Kibaha kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo ifikapo juni 25 mwaka huu .
Akizungumza wakati alipotembelea ujenzi unaondelea katika halmashauri za wilaya ya Kibaha,Ndikilo aliwataka baadhi ya wanasiasa na watendaji kukwamisha kwa namna yoyote miradi ya kitaifa na kimkoa kwa maslahi ya matumbo yao .
Alisema ,katika kukabiliana na changamoto ya utoaji wa huduma ya afya kwa jamii serikali ya awamu ya tano inajenga hospitali za wilaya tatu za kisasa ,mkoani hapo ambazo zitagharimu kiasi cha sh. bilioni 4.5.
Ndikilo alielekeza, fedha zote zinazoelekezwa katika miradi hiyo muhimu zitumike kwa wakati na kwa matumizi lengwa bila kuziacha kubaki viporo.
“Uzoefu tulioupata kwamba kwanini tunachelewa chelewa sana ni baadhi yetu kutaka fedha hizi ,hii hii bilioni 1.5 kwa kila halmashauri wanajiwekea nipate asilimia 10, fundi wangu ,mjomba wangu apate tenda ya ufundi ,ndugu yangu alete matofali na kutusababishia kuchelewa malengo yetu”alifafanua Ndikilo.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alieleza changamoto kubwa iliyosababisha kuchelewa kidogo kwa ujenzi ni hali ya mvua hivyo wanaomba kuongezwa muda japo siku 20 badala ya juni 25 mwaka huu.
Awali kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Suzan Chaula ,alielezea wanajenga majengo saba ambapo ujenzi wa majengo yote umefikia asilimia 55.
Suzan aliiomba serikali iwaongezee fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo awamu ya pili na ununuzi wa vifaa kwenye majengo hayo .