Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye Mradi wa Maji wa Manga katika Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi pamoja na viongozi wa mkoa wa Katavi na wataalam wa Sekta ya Maji mkoani Katavi.Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye Mradi wa Maji wa Manga katika Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi pamoja na viongozi wa mkoa wa Katavi na wataalam wa Sekta ya Maji mkoani Katavi.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa Mkoa wa Katavi kuhusu mgao wa fedha katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera wakitoka kuangalia chanzo cha maji cha Mradi wa Maji wa Iklongo II, Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera wakitoka kuangalia chanzo cha maji cha Mradi wa Maji wa Iklongo II, Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA), Mhandisi Zacharia Nyanda akitoa maelezo kuhusu Mradi wa Maji wa Ikolongo II uliopo Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.
…………………………………………………………….
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesisitiza umuhimu wa Wataalam wa Sekta ya Maji kusimamia miradi ya maji kwa ufanisi ili kuweza kuwa na miradi yenye tija inayolingana na thamani ya fedha zinazowekezwa na Serikali kwenye miradi yote nchini.
Profesa Mbarawa amesema ni lazima kuwe na usimamizi mzuri kwa kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya maji, ili kuweza kupata matokeo yanayotarajiwa baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, ambayo ni kumaliza tatizo la maji nchini kote.
Akitoa majibu kwa mkandarasi aliyekuwa akilalamika kucheleweshewa malipo na Serikali, Profesa Mbarawa amesema jambo hilo linatokana na tabia ya wakandarasi kuweka makisio makubwa ya gharama za miradi ya maji kwa dhumuni la kupata faida kubwa, kulinganisha na gharama halisi za ujenzi wa miradi hiyo. Wakandarasi wengi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wahandisi wasio waaminifu kuihujumu Serikali na kusababisha kushindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kutokana na gharama kuwa kubwa kupita kiasi.
“Tumegundua tulikuwa tukiibiwa fedha nyingi, hivi sasa tumeweka utaratibu wa kujiridhisha na makisio ya gharama za kila mradi kwa kila kipengele, kabla ya kuingia mkataba. Hatua hii imetusaidia kupunguza gharama kwa kulipa gharama zinazostahili. Hivyo, kutuwezesha kulipa wakandarasi kwa wakati na kuwa na miradi yenye viwango bora inayokamilika kwa wakati’’, Profesa Mbarawa amesema.
Akiwa wilayani Mpanda, Profesa Mbarawa amekagua mradi wa maji wa Manga-Kasokola ulioanza kutekelezwa Februari, 2018 chini ya Mkandarasi Monmar & Sons Co. Ltd Building and Civil Engineering na utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2019. Lengo la mradi huu ni kufikisha huduma karibu na wananchi wa Manga na Kasokola wapatao 7,560 kwa umbali usiozidi mita 400.
‘‘Kwa ujumla nimeridhishwa na maendeleo ya miradi ya maji katika mkoa wa Katavi, kikubwa ni kuweka msukumo mkubwa ili miradi hii iweze kukamilika mapema zaidi ili matokeo ya miradi hii iweze kuonekana kwa wananchi wa mkoa huu’’, Profesa Mbarawa amesema.
Profesa Mbarawa ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Katavi kwa kutembelea miradi ya maji ya Manga, Ikolongo II, Igagala, Ngomalusambo na Kabungu katika Wilaya za Mpanda, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda na Tanganyika.