Wakati Serikali ikiwataka Wananchi wote kusalimisha kwa hiari mifuko ya plastiki waliyonayo kabla ya Juni mosi mwaka huu, Ofisi ya Tarafa ya Mihambwe imesema hakutakuwa na mzaha kwa watakaopuuza kutii agizo hilo.
Msimamo huo umetolewa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kwenye mkutano wa Kijiji cha Namunda kilichopo kata ya Kitama akiwataka kuonyesha ushirikiano kwa kusalimisha mifuko ya plastiki kwa hiari kabla ya msako haujaanza.
Gavana Shilatu alisema kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na mifuko ya plasitiki iliyotapakaa kila kona na kuathiri sana makazi na maeneo ya viumbe hai .
*”Onyesheni ushirikiano kutokomeza mifuko ya plasitiki. Mwenye akiba ya mifuko hiyo aisalimishe ofisi ya Kijiji au ofisi ya kata. Watendaji na viongozi hakikisheni agizo hilo la Serikali linatekelezwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”* Alisema Gavana Shilatu.
Gavana Shilatu alisema plasitiki zinaathari kubwa kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vyote hivyo uamuzi wa Serikali unahitaji kuungwa mkono na kutekelezwa kwa wakati muafaka.
Kwenye mkutano huo wa siku ya pili, Mwenyekiti wa Kijiji Cha Namunda (CUF) Suleiman Mkubulu aliwaomba radhi wanakijiji kutokana na uzembe uliojitokeza kwenye miradi ya maendeleo tangu achaguliwe kushika wadhifa huo
“Nimekubali makosa na lawama dhidi yangu .Nataka tusameheane.” alisema Mkubulu huku baadhi ya Wanakijiji wakipokea ombi lake shingo upande na wengine wakitaka ajiuzulu nafasi yake.