Mmoja wa viongozi wa dini, mchungaji Christosiler Kalata kutoka KKKT- Dayosisi ya Mashariki na Pwani akichangia mada katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama
Orsolina Tolage, kutoka Wizara ya Afya ( kitengo cha Elimu ya Afya Kwa Mama) akitoa mada katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama
Mtaalam wa Mawasiliano kutoka UNICEF, Usia Nkoma akitoa mada katika semina ya kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama
Waandishi wa Habari na watangazaji kutoka mikoa mbalimbali wakiwa katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyomaliza Jana
………………………………………….
Semina tatu zilizoandaliwa na Kampuni ya True Vision Production (TVP) kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ kwa wahariri, viongozi wa dini na waandishi wa habari zimemalizika katika Hotel ya Regency, jijini Dar es Salaam.
Semina hizo zilikuwa na lengo la kuelimisha makundi haya matatu (wahariri, viongozi wa dini na waandishi) juu ya umuhimu wao wa kushiriki katika kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ yenye lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto.
Tahseen Alam, Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka UNICEF Tanzania amesema serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika miaka 10 iliyopita ya kuokoa vifo vya mama na mtoto, ikiwemo eneo la chanjo ambapo watoto wengi na mama wajawazito wanapatiwa.
Lakini kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mtaalamu wa Mawasiliano mwenzake kutoka UNICEF, Usia Nkoma, Tanzania bado ina safari ndefu ya kutokomeza vifo hivyo kwa sababu ni nchi ya tisa kati ya nchi 10 duniani zinazoongoza kwa vifo vya mama wajawazito na watoto.
Takwimu zinaonyesha mama wajawazito wasiopungua 6000 (wastani 8,000) wanakufa kila mwaka wakati wanajifungua, sawa na wanawake 556 kwa kila vizazi hai 100,000.
Pia asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka mitano (5) pia wanakufa ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa, asilimia 40 kati ya hawa wakiwa watoto wachanga.
Wakizungumza tofauti tofauti katika semina hizi, mmoja wa waandishi na wahariri wakongwe nchini, Theophil Makunga amasema takwimu hizi zinatisha, hivyo kuna haja kwa wahariri kuzipa kipaumbele habari zinazohusu wanawake wajawazito na watoto ili kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchukua hatua kupunguza vifo hivi.
Naye Sheikh Hamid Jongo wa msikiti wa Manyema amesema kuna haja ya kuwafunda watumishi wa afya , kwani baadhi yao inasemekana hawana lugha rafiki kwa wagonjwa.
Kauli yake imeungwa mkono na Christosiler Kalata, mchungaji kutoka KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ambaye amehimiza wahudumu wa Afya kuzingatia miiko ya taaluma yao ili kuhakikisha vifo vya mama wajawazito na watoto vinaisha.
“Tutahakikisha, kama waandishi wa habari tunabadili mtazamo wa kazi zetu kwa kuzipa kipaumbele habari zinazohusu afya ya mama wajawazito na watoto, kama ilivyo kwa habari nyingine,” amesema Tumaini Msowoya, kutoka gazeti la Mwananchi.
Washiriki wote wa semina hizi tatu wameishukuru kampuni ya True Vision Production, UNICEF Tanzania na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kwa kuhakikisha kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ inafanikiwa, kwani jukumu la kupunguza vifo na kila mmoja katika jamii.
Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya Taifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.
Madhumuni ya Serikali ni kuhamasisha viongozi wake, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya serikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujumla kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.