Na Subira Kaswaga (Afisa Habari NEC)
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanya uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum saba (07) katika Hamlashauri za Manispaa za Sumbawanga na Tunduma, Halmashauri za Wilaya za Tandahimba, Korogwe na Rombo.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji (R) Mbarouk S. Mbarouk amesema kuwa, uteuzi huo umefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa juu ya uwepo wazi wa nafasi za Madiwani Wanawake wa Viti Maalum katika halmashauri hizo kutokana na sababu mbalimbali.
Amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na waliokuwa Madiwani katika Halmashauri hizo kufariki dunia, kujiuzulu na kuvuliwa uanachama na hivyo nafasi zao kuwa wazi.
Jaji (R) Mbarouk S. Mbarouk amewataja Madiwani walioteuliwa na vyama wanavyotoka kuwa ni Regina Willbard Lyakurwa na Beatrisi Revocatus Silayo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Regina Abiudi Liffi Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na Agness Atanazi Chilulumo Halmashauri ya Manispaa ya Tunduma wote wanatoka CHADEMA.
Wengine ni Shahara A. Alfani na Mey R. Dadi Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kutoka CUF na Mwajuma Waziri Kitumpa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutoka CCM.